Tuesday, August 7, 2012

Kipigo cha Dk. Ulimboka chazua balaa Tigo

Best Blogger Tips
 KUTEKWA, kupigwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka na hatimaye kufungiwa kwa Gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kumeleta kizaazaa katika kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Habari kutoka ndani ya kampuni hiyo ya simu yenye mtandao mpana nchini, zinasema kuwa zaidi ya wafanyakazi 30 wamefukuzwa kazi na wengine wako kwenye uchunguzi wakituhumiwa kuvujisha mawasilino ya siri ya simu za wateja kwa Gazeti la MwanaHalisi.

Kwa mujibu wa habari hizo, taarifa za mawasiliano za simu zinazodaiwa kuvujishwa na wafanyakazi hao, zilikuwa kati ya Dk. Ulimboka, Afisa Usalama wa Ikulu na watu aliowasiliana nao kabla ya kutekwa.

Rais Jakaya Kikwete amepata kuliambia taifa mara mbili kwa njia ya televisheni, mwishoni mwa Juni na alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari wiki iliyopita, kwamba serikali yake haihusiki kuteka, kutesa na kumtupa daktari huyo porini.

Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda amepata kuliambia Bunge kuwa, serikali yake haihusiki na utekaji, utesaji na kuhoji, “...serikali imteke ili iweje?”

Hivi karibuni serikali ililifungia Gazeti la MwanaHalisi baada ya kuandika habari iliyomtaja ofisa mmoja wa Idara ya Usalama wa Taifa Ikulu (TISS), kuwa ndiye aliyetekeleza mpango wa kumteka, kumpiga na kumtesa hadi kumjeruhi Dk. Ulimboka, ambaye kwa sasa anaendelea na matibabu kwenye hospitali moja nchini Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa habari hiyo ambayo serikali inadai kuwa ni ya uchochezi, MwanaHalisi ilianika namba ya simu ya ofisa huyo pamoja na watu wengine wanaodaiwa kuhusika katika tukio hilo linaloendelea kuchunguzwa na kamati maalumu iliyoundwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).

Vyanzo vya habari kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi waliokumbwa na sekeseke hilo, zinasema kuwa waliofukuzwa wengi ni wafanyakazi wa kitengo cha IT ambao wanadaiwa kuhusika kutoa taarifa za siri ya mawasilino kati ya Dk. Ulimboka na watu wanaoaminika kuwa ni wabaya wake.

Mmoja wa wafanyakazi kutoka Kampuni ya Tigo, aliliambia gazeti hili kuwa mbali na kutuhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, wafanyakazi wengine wametimuliwa kwa madai ya kufanya udanganyifu kwenye huduma za Tigo Pesa na kujipatia fedha.

“Kweli watu wengi wamefukuzwa wakituhumiwa kutoa siri kwa Gazeti la MwanaHalisi, lakini wengine walikuwa wakishirikiana na mawakala wa Tigo Pesa kuiibia kampuni.

“Kwa mfano mfanyakazi alikuwa anakubaliana na wakala kumwingizia kiasi kama cha sh milioni moja, lakini anaweza kuingiza hadi sh milioni 1.5 na kati ya hizo sh 500,000 ni mali yake,” alisema mfanyakazi huyo.

Akizungumzia na Tanzania Daima Jumatano, Mhariri Mkuu wa Gazeti la MwanaHalisi, Jabir Idrissa alishangazwa na taarifa za Tigo kuwafukuza wafanyakazi wake kwa sababu ya habari iliyochapishwa na gazeti lake.

“Chanzo chetu cha habari hakikutoka kwa wafanyakazi wa Tigo. Kama wamefukuzwa kwa sababu ya MwanaHalisi, wamewaonea bure. Kama Tigo ndio waliotupa taarifa na zile za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), zilitoka wapi?” alihoji Jabir na kusisitiza wafanyakazi hao wameonewa bure.

Ofisa Uhusiano wa Tigo, Edward Shila, alipohojiwa kuzungumzia tukio hilo, hakukubali wala kukataa madai hayo na kumtaka mwandishi kumtumia maswali kupitia e-mail yake ili aweze kuyatolea majibu kiofisi.

“Kama una maswali naomba uniandikie kupitia e-mail yangu ambayo nakutumia sasa hivi…maana siko tayari kutoa kauli yoyote isiyokuwa ya kiofisi,” alisema.

Naye Omary Matulla ambaye amejitambulisha kuwa ni ofisa wa kitengo cha kumbukumbu katika kampuni hiyo, alikanusha kuwapo kwa taarifa za kufukuzwa wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Alisema kuwa kila mfanyakazi ana mipaka ya kufanya kazi katika kampuni hiyo, na pia ni wajibu wa kila mtumishi kutunza siri kubwa.

“MwanaHalisi ana mbinu zake za kupata habari wala haiwezekani kupata habari kupitia kampuni yetu na hata hivyo jambo hilo si rahisi hata kidogo kutokea,” alikanusha Omary.

Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Tangu kutokea kwa tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wamekuwa wakiinyoshea kidole serikali kwamba ndiyo iliyohusika.

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Polisi mkoani Dar es Salaam, Suleiman Kova, hivi karibuni alitangaza kumfikisha mahakamani mtu mmoja aliyedai kukiri kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka.
Kova aliwaambia waandishi wa habari kuwa, polisi wamekamata mtu aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka.

Alidai kuwa mtuhumiwa alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe, Dar es Salaam.
Lakini hata hivyo, mchungaji wa kanisa hilo, Josephat Gwajima alikana kauli ya Kova juu ya mtuhumiwa huyo, akisema hajakwenda kutubu kwao.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits