Friday, August 3, 2012

UWT ni Kilango vs Sophia Simba

Best Blogger Tips
 Vita kubwa ya kuwania uenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeonekana dhahiri, baada ya vigogo wawili wenye nguvu kuchukua fomu za kuwania kiti hicho.

Kuwepo kwa vita kali katika kinyang’anyiro hicho kunatokana na kujitokeza kwa Mbunge wa Same Mashariki, Anne-Kilango Malecela, kuchukua fomu hizo jana.

Mwenyekiti wa sasa wa UWT Taifa, Sophia Simba, juzi alikuwa wa kwanza kuchukua fomu hizo kutetea nafasi yake katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Kilango ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, alichukua fomu hizo akiwa ameongozana na mumewe ambaye ni mwanasiasa mkongwe nchini na ndani ya CCM, Mzee John Malecela.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana baada ya kukabidhiwa fomu na Katibu Msaidizi Mkuu wa UWT,  Martha Kanakamfumo, Kilango alisema ameamua kugombea nafasi hiyo ya juu kisiasa ndani ya CCM kwa kuwa ana uwezo wa kuwaandaa wanawake kiuchumi na kisiasa.

“Wanawake katika ngazi ya wilaya wanapaswa kuandaliwa wawe kuwa na nguvu za kiuchumi na kisiasa ili wapate na uwezo kutembea nyumba hadi nyumba nyakati za uchaguzi na kukiletea chama chetu ushindi,” alisema Kilango.

Kuhusu uzoefu wake ndani ya UWT, Kilango alisema amewahi kuwa mwenyekiti wa umoja huo katika ngazi ya wilaya.

“Uwezo wangu wa kisiasa umetokana na uongozi wa Mwenyekiti wa UWT ngazi ya wilaya, Wilaya ya Kinondoni. Kwa kifupi nguvu yangu ya kisiasa inatoka ndani ya tumbo la UWT,” alisema Kilango.

Simba ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, alichukua fomu hizo juzi asubuhi katika ofisi za UWT mjini hapa.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu hizo Simba, alisema ameamua kutetea nafasi hiyo kwa mara nyingine ili amalizie mambo aliyoyaanza wakati wa uongozi wake, ikiwemo ujenzi katika viwanja mbalimbali vya umoja huo nchini.

“Kutokana na uzoefu nilioupata miaka minne iliyopita, tumekuwa kitu kimoja katika kipindi chote, wanawake wenzangu wamenipa ushirikiano mzuri wakati wa utekelezaji wa majukumu yangu ndiyo umenihamasisha kugombea kwa mara nyingine nafasi hii,” alisema Sophia.

Sophia alisema katika kipindi chake cha uongozi, anajivunia kutembelea mikoa yote nchini na kuzungumza na wanawake  kuhusiana na mambo mbalimbali ya maendeleo.

Sophia alisema iwapo atachaguliwa kuongoza kwa mara nyingine jumuiya hiyo, ataendeleza waliyoyaanzisha ikiwemo Chama cha Ushirika wa Kuweka na Kukopa (Saccos) ambacho kitazinduliwa Septemba, mwaka huu.

Ingawa bado vigogo zaidi hawajajitokeza kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo, lakini kujitokeza kwa Sophia kutetea nafasi yake na Kilango kujaribu kwa mara ya kwanza, ni sababu tosha za kukifanya kinyang’anyiro hicho kuwa na ushindani wa hali ya juu.

Hali hiyo inatokana na Sophia kuwa na ushawishi kwa wajumbe wengi akiwa kama mwenyekiti na vile vile kuungwa mkono na vigogo wa juu wa chama hicho akiwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC).

Kwa upande wake, Kilango siyo mtu wa kupuuzwa kwa kuwa pia kama mbunge na mjumbe wa NEC, ana ushawishi mkubwa na vile vile anaweza kunufaika kutokana na umaarufu wa mumewe ambaye ni Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Makamu Mwenyekiti Bara na mjumbe wa kudumu wa NEC na CC.

Katika uchaguzi uliopita uliomwingiza madarakani, Sophia alimshinda Janeth Kahama, mke wa mwanasiasa mkongwe nchini, George Kahama, huku ukiwemo ushindani mkali.

Kimsingi, nafasi ya uenyekiti wa UWT ni nyeti sana ndani ya chama hicho kwa kuwa mwenyekiti anakuwa mjumbe wa NEC na CC moja kwa moja, ambavyo ni vikao vya kufanya mamuzi makubwa ya chama.

Kwa mfano, kinyang’anyiro hicho kitakuwa ni mwelekeo wa kupanga safu za uongozi wa chama na dola kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2012.

Kwa kujibu wa ratiba ya uchaguzi huo, uchukuaji wa fomu kwa ajili ya uchaguzi huo utaendelea hadi Agosti 6, mwaka huu.

Chanzo: Ippmedia

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits