Friday, April 1, 2011

Best Blogger Tips
Adam Lusekelo afariki dunia

 

MWANDISHI mahiri nchini, Adam Lusekelo (54), amefariki dunia usiku wa kuamkia jana wakati alipokuwa anakimbizwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa matibabu, mke wa marehemu Scolastica Lusekelo amebainisha jana.

Alisema afya ya marehemu ilidhoofu usiku wa juzi na waliamua kumpeleka hospitali ya Aga Khan, lakini nao walikata shauri na kumhamishia Muhimbili na mauti ilimfika akiwa njiani kupelekwa hospitali hiyo ya rufaa.

“Oh, no! Tumempoteza kipenzi cha wasomaji wa gazeti la ‘Sunday News’,” alisema kwa masikitiko Mhariri Ichikaeli Maro mara baada ya kupokea taarifa za kifo cha Lusekelo.

Lusekelo atakumbukwa na wasomaji wa magazeti ya serikali ya Sunday News alikokuwa akichangia kwenye safu ya A Light Touch na HabariLeo kwenye safu ya Chombezo la Lusekelo.

Safu zake zilikuwa na utofauti kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuandika masuala muhimu ya kitaifa kwa lugha laini, jambo ambalo liligusa mioyo na nafsi za wapenzi wake.

“Mume wangu atapungukiwa na kitu kwa sababu alikuwa mpenzi sana wa safu ya Lusekelo,” alisema Joyce Sabuni, mfanyakazi wa Tanzania Standard Newspapers (TSN) inayochapisha magazeti ya DAILY NEWS, SUNDAY NEWS, HABARILEO na HABARILEO Jumapili, katika kitengo cha usambazaji.

Kaimu Mhariri Mtendaji wa TNS, Mkumbwa Ally ni miongoni mwa watu walioguswa na msiba wa kifo cha mwandishi huyo mkongwe aliyekuwa na kipaji cha hali ya juu katika fani ya uandishi wa habari.

Kaka wa marehemu, Ben Mwakang’ata alisema mipango ya mazishi inafanywa nyumbani kwake Ubungo na kuwa upo uwezekano mwili wa marehemu ukasafirishwa kesho kuelekea Rungwe, mkoani Mbeya.

Marehemu Lusekelo ameacha mke na watoto watatu, wakiwemo wawili wa kike.

Katika uhai wake alifanya kazi TSN kwa muda mfupi katika miaka ya 1980 kabla ya kujiunga na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kama mwandishi wa habari akiandikia akiwa Dar es Salaam.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits