Monday, April 11, 2011

Best Blogger Tips
Mkama kuvaa viatu vya Makamba

Via HabariLeo

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza safu yake mpya ya uongozi wa juu akiwemo Katibu Mkuu mpya, Kamati Kuu na Sekretarieti mpya.

Katibu mpya wa CCM wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ameitangaza safu hiyo usiku huu katika ukumbi wa Halmashauri Kuu ya CCM mjini Dodoma muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.

Katika mabadiliko hayo makubwa ya uongozi CCM, Wilson Mkama ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM kuchukua nafasi ya Yusuf Makamba.

Mkama amekuwa kiongozi kwa muda mrefu Serikalini , na kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Magazeti ya Serikali ya Tanzania Standard Newspapers (TSN).

Aliyekuwa Katibu wa Uenezi na Itikadi CCM, John Chiligati sasa anakuwa Naibu Katibu Mkuu CCM Tanzania Bara kuchukua nafasi ya George Mkuchika.

Naibu Katibu Mkuu mpya wa CCM Zanzibar ni Vuai Ali Vuai, Januari Makamba anakuwa Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.

Mwigulu Mchemba anakuwa Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, Aisha Abdallah Juma anakuwa Katibu wa NEC Oganaizeshi, na Nnauye anakuwa Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi.

Kwa mujibu wa Nnauye, Kamati Kuu mpya ya CCM ina wajumbe 14, wajumbe kutoka Tanzania Bara ni Abdulrahman Kinana, Zakia Megji, Abdallah Kigoda, Pindi Chana, Stephen Wassira, Costansia Bugie na William Lukuvi.

Wajumbe kutoka Zanzibar ni Dk. Hussein Mwinyi, Dk. Maua Daftari, Samia Suluh Hassan, Shamsi Vuai Nahodha, Omary Yusuf Mzee, Profesa Mnyaa Mbarara, na Mohamed Seif Khatib.

Katika kujiimarisha, Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho, amewateua wajumbe saba wa NEC ili kukamilisha idadi ya wajumbe 10 anaoruhusiwa kuwateua.

Walioteuliwa ni Anna Abdallah, Peter Kisumo, Mwigulu Mchemba, Januari Makamba, Wilson Mkama, Ali Juma Shamhuna, na Dk. Emmanuel Nchimbi.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits