Tuesday, April 5, 2011

Best Blogger Tips
Maajabu mapya Loliondo

*Mwizi wa fedha, simu apambana na muujiza
*Apigwa ganzi ya macho, atoa mali alizoiba

MAAJABU yanaendelea kutokea kwa Mchungaji Mstaafu Ambilikile Masapila, katika Kijiji cha Samunge, Loliondo; na safari hii ni kwa kijana anayetuhumiwa kuiba fedha na simu.

Kijana huyo aliyejulikana kwa jina moja la Joseph (28), alituhumiwa kuiba Sh 20,000 za Kenya, Sh 80,000 za Tanzania, simu na vitu kadha wa kadha kutoka katika gari walimokuwa raia wa Kenya.

Raia hao wa Kenya walifika kijijini Samunge kunywa dawa.

Wizi huo ulifanyika Aprili 2, mwaka huu, usiku baada ya watu wasiojulikana kuwapekua raia hao wa Kenya.

Taarifa zilimfikia Mchungaji Masapila na akatoa karipio akitaka vitu vilivyoibwa virejeshwe kwa wenyewe haraka.

Baada ya Ibada ya Jumapili Mchungaji Masapila alielekea hadi kwenye eneo ambalo amekuwa akitolea dawa na kuutangazia umma kuhusu taarifa za kuwapo wezi.

“Ndugu zangu wagonjwa, Kijiji cha Samunge tumevamiwa na majambazi, wezi ambao wamewaibia watu nawaomba waliofanya kitendo hicho kurejesha haraka vitu hivyo kabla Mungu hajaanza kuwaadhibu kwa mkono wake,” alinukuliwa akisema.

Alisema endapo aliyeiba angesita kurejesha mali alizoiba, basi umma ungemshangaa na kumtambua kwa matendo yake.

Ilielezwa kuwa ndani ya dakika 15 hivi, mama aliyekuwa na kijana mmoja (Joseph) alisikika akiomba msaada kwa kijana wake kwamba alikuwa akilalamika kupigwa na watu asiowaona.

Baada ya Mchungaji kumuona kijana huyo alimwamuru asalimishe vitu alivyokuwa ameiba ili ampatie dawa.

Kijana huyo aliendelea kulalamika kuwa amepoteza nuru, na wakati huo huo alianza kutoa vitu alivyokuwa ameiba.

Alitoa simu aina ya Blackberry, Sh 20,000 za Kenya, hati ya kusafiria na Sh 80,000 za Tanzania.
Umati ulipigwa butwaa, na kisha Mchungaji Masapila alimwangia dawa mwilini na kumwamuru aondoke eneo hilo haraka. Kijana huyo alianza kuondoka huku akiomba msamaha.

Kijana alitambuliwa kuwa ni mkazi wa Mkoa wa Singida. Hata hivyo, alipandishwa kwenye basi lililokuwa likienda Shinyanga.
Source: Newhabari

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits