Wednesday, April 13, 2011

Best Blogger Tips
Namkuta Adamu Lusekelo 'Ninja'

Makala ya Fred Macha

LABDA si wasomaji wengi wa Kiswahili wanaomfahamu mwandishi wa habari wa siku nyingi aliyefariki dunia wiki iliyopita, Adam Lusekelo Mwakang’ata.

Nilimfahamu Lusekelo mwaka 1970 wakatu tunasoma wote  sekondari. Tulimkatia jina la mbabe mpiganaji, yaani Njinja Maloni. Adam “Njinja” alikuwa bondia  na baadaye kujifunza Shotokan karate ( toka Korea) wakati akisomea uandishi wa habari, Nairobi. Aliwahi pia kupanda  mlima Kilimanjaro mara kadhaa.

Bahati mbaya alipoacha mazoezi na kujisahau (kwa pombe kupindukia ) akakumbwa na kisukari. Nikiwa rafiki yake wa utotoni  nilishtuka nilipomwona alivyokonda  mara ya mwisho mwaka juzi, mjini Dar es Salaam.

Ulikuwa mfano wa tabia yake ya masihara yaliyojaa ujumbe. Usingeacha kucheka ulipokutana na  Adam Lusekelo. Alikuwa chizi kupindukia na ucheshi wake ulijionyesha katika mamia ya makala za kejeli alizoziandika   katika safu ya “With A Light Touch.”
 Miaka ya mwisho alifungua pia blogu (“Adam Lusekelo On Line”) aliyoendeleza mada zake. Adam Lusekelo hakuwa mwoga. Ingawa marehemu babake alikuwa zamani katika serikali (tulipofahamiana 1970, Mzee Aaron Mwakang’ata, alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha), Adam hakuhofia kuwasakama viongozi mafisadi. Kinyume cha baadhi ya watoto wa vigogo wanaofunga macho na kufaidi matunda ya wazazi wao, alitumia nafasi hiyo kukemea ufuska.

Novemba 14, 2010 aliandika : “Jini Hatimaye Limeamka” ..akichambua  namna vijana wa Kitanzania walivyochoshwa na wanasiasa waongo.
“Hao wanaolifanya Bunge hoteli ya kupangisha yenye hewa safi ya baridi itabidi waamshwe na kupigwa mateke makalioni. ”
Adam aliandika mada za kila aina, ikiwemo kumshauri mwigizaji Steve Kanumba aliyesutwa kwamba hajui Kiingereza alipoingia Big Brother Afrika Kusini, 2009. Kinachofurahisha, makala hii  ni namna anavyochangamsha hoja akitumia Kiingereza chepesi. Kinyume cha waandishi wanaojifaragua kwa lugha ya mawe, iliyojaa maneno magumu, aliandika sentensi fupi za utani, utani...

Anamkumbusha Kanumba juu ya watu wengi kukuonea wivu hasa mtu anapofaulu katika maisha. “Ukibahatika kufahamika, wapambe watataka kuimanya hata rangi ya chupi yako,” anasema.

Hata mwanamke unayekwenda naye atachunguzwa.  “Wataanza kusema sura yake mbaya kama jini, kwamba miguu yake mirefu kama ya twiga. Ndo’ ubinadamu huo.”
Adam Lusekelo aliendeleza lugha ya uandishi Tanzania akitumia Kiingereza safi chenye utamaduni wa Afrika Mashariki. Unapokisoma Kiingereza chake ni kama kumsikiliza Mswahili akiongea lugha fasaha ya kigeni bila kujisahau atokapo. Anakumbusha enzi  Mzee John Malecela alipokuwa balozi wetu Umoja wa Mataifa akiongea Kiingereza fasaha  cha lafidhi ya Kigogo na Kiswahili. Siri ya ujuzi wake nini?
 Kila nilipoongea naye, Adam, hakuacha kunitajia kitabu fulani alichokuwa akisoma; alikuwa mwanafunzi mzuri wa fasihi na lugha, jambo linalozidi kudhoofika miongoni mwa waandishi chipukizi leo Bongo.
Endelea kusoma habari hii.................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits