Monday, October 24, 2011

Gaddafi dikteta mwenye mafanikio, wosia wake waanikwa

Best Blogger Tips
SIKU chache baada ya  kuuawa kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, walibya na dunia kwa ujumla imeingia katika mitizamo tofauti kuhusu kiongozi huyo huku wengi wakikumbuka mafanikio aliyoleta kwa taifa hilo tofauti na viongozi wengine waliong’olewa kwa udikteta.Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikimtangaza na kutafuta namna zote za kujenga picha ya udikteta bila kuangalia upande wa pili wa Libya iliyooachwa  na Gaddafi.

Baadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakizungumziwa ni iwapo Libya ya sasa itaweza kuneemeka na kile ambacho ilikuwa ikipata kutoka kwa kiongozi huyo, ambaye  hivi karibuni  aliuawa na wapinzani wake.

Gaddafi, tofauti na viongozi wengine waliowahi kutajwa kuwa madikteta  duniani,  ana mengi ya kukumbukwa na kusifiwa kwayo.Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuongozi wamekuwa wakieleza kusikitishwa kwao na kutotambua aina ya demokrasia ambayo baadhi ya watu wa Libya wanaililia kwa sasa na iwapo itaboresha au kuharibu kabisa maisha yao.

Hii inawekwa wazi kwamba  pamoja na kwamba Gaddafi ametumia fedha nyingi za Libya katika masuala binafsi,  lakini je, kwa wastani Libya ni maskini? Wapo viongozi waliozitumia nchi zao na kuziharibu kabisa, Gaddafi aliwahi kuifilisi Libya?

Haya ni baadhi ya mambo ambayo Gaddafi  aliyasimamia na kuyatekeleza katika utawala wake wa miaka 42 kwa Libya.Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na tovuti za mawasiliano za Libya na Zimbabwe zimeeleza kuwa nchini Libya hakuna mwananchi aliyewahi kulipa bili ya umeme, umeme ulikuwa bure kwa raia wake wote.

Hakukuwa na riba katika mikopo, benki zote Libya zilikuwa chini ya Serikali,  mikopo ilitolewa kwa wananchi bila riba ya kiasi chochote .
Taarifa hizo zikafafanua kuwa makazi ni haki ya msingi nchini Libya, Gaddafi aliwahi kusisitiza kwamba wazazi wake hawawezi kupata makazi hadi kila raia apate makazi. Baba wa Gaddafi alifariki dunia wakati yeye, mama yake wakiwa wanaishi katika hema.

Wanandoa wote wapya nchini humo walipata Dola 50,000 kwa Serikali kwa ajili ya kununua makazi yao kuwasaidia kuanzisha familia mpya.Elimu na huduma za  kiafya vilitolewa bure. Wakati Gaddafi nachukua nchi  asilimia ya waliokuwa na elimu ilikuwa 25, kwa sasa inafikia  83.
Kwa waliotaka kuwa wakulima, walipewa ardhi bure, nyumba katika shamba lao, vifaa, mbegu na mifugo kwa ajili ya kuanzisha miradi.Iwapo kuna waliokuwa hawawezi kupata huduma za elimu na afya wanazostahili, Serikali iliwalipia kwa ajili ya kuzipata nje ya nchi, hizi hazikuwa bure, walitakiwa kuchangia, walipata Dola2,300 kwa mwezi kwa ajili ya makazi na usafiri.

Kwa waliokuwa wakitaka kununua magari,  Serikali ililipia kwa asilimia 50 ya bei. Bei ya petroli ilikuwa karibu na bure, lita ililipiwa kwa Dola 0.4.
Libya haidaiwi nje, pia ina akiba inayofikia Dola150 bilioni nje ambayo kwa sasa imezuiliwa.Kwa waliomaliza vyuo,  Serikali iliwapatia posho sawa na mshahara wa maofisa hadi watakapopata ajira yenye uhakika. Sehemu ya mauzo ya mafuta ya Libya iliwekwa moja kwa moja kwenye akaunti ya raia wake.

Kila mwanamke aliyejifungua alipata posho ya Dola5000, mikate 40 iliuzwa kwa dola0.15,  asilimia 25 wa Walibya, wana shahada ya chuo kikuu.Kama hiyo haitoshi taarifa hizo zimeeleza kuwa alisimamia mradi mkubwa kabisa wa umwagiliaji, uliopewa jina la Great Man-made River, kuhakikisha maji yanakuwepo kwenye maeneo yote ya nchi yenye jangwa.

Wakati wa vikwazo kwa Serikali yake miaka ya 1980, Libya ilikuwa miongoni mwa nchi tajiri kabisa kwa msingi wa pato la ndani, ikwa na kiwango cha juu cha maisha kuliko Japan. Ilikuwa ni nchi tajiri kuliko zote kabla ya vuguvugu la mapinduzi.
Wastani wa kiwango cha maisha kwa pato la kichwa ni Dola11,314 . Gaddafi amewahi kutumia fedha nyingi kwa ajili ya safari zake na miradi yake, lakini amefanya mabo makubwa ambayo hakuna dikteta aliyewahi kuyafanya kwa watu wake. Alirejesha pato kwa watu wake, aliwajali.

          Wosia wa Gaddafi kabla ya kifo
Katika wosia wake, Kanali Gaddafi aliwaasa wafuasi wanaomuunga mkono kuendelea kupambana.
Alielezea msimamo wake kuwa amechagua kupambana hadi hatua ya mwisho na kufia katika ardhi ya Libya kuliko kuchagua njia nyepesi, ambayo kwa mtizamo wake,  ni kitendo cha kujidhalilisha kisichokuwa na heshima, kukimbilia uhamishoni nje ya nchi yake, ambapo tayari alishapata ahadi nyingi za ulinzi.

Katika lugha ya Kiingereza, waraka wake wa wosia umetafsiriwa ukisomeka: “Hii ni hiyari yangu. Mimi Muammar bin Mohammad bin Abdussalam bin Humayd bin Abu Manyar bin Humayd bin Nayil al Fuhsi Gaddafi, ninaapa kwamba hakuna Mungu mwingine zaidi ya Allah na Muhammad ni Mtume wake, amani iko kwake. Ninaahidi nitakufa nikiwa Muislamu.

 “Iwapo nitauawa, nitapenda kuzikwa kwa mujibu wa taratibu za kiislamu, nikiwa nimevaa mavazi nitakayokuwa nimevaa wakati kifo change kikitokea, bila mwili wangu kuoshwa, katika makaburi ya Sirte, jirani na familia na jamaa zangu.

“Nitapenda kwamba familia yangu, hasa wanawake na watoto, watunzwe vyema baada ya kifo changu. Watu wa Libya wana wajibu wa kulinda wasifu, mafanikio, historia na heshima ya waasisi na mashujaa wake.

“Watu wa Libya hawatakiwi kupuuza kujitapa na lazima wawe  watu huru wa kuthaminiwa. Ninawataka wale wanaoniunga mkono kuendelea kupambana, kuwakabili wote wanaosimama kutoka nje dhidi ya Libya, leo, kesho na siku zote.

 “Hata kama hatutashinda mapema, tutatoa funzo kwa vizazi vyetu vijavyo, kwamba kuchagua kulinda utaifa ni heshima na kuliuza ni uasi mkubwa ambao historia haitausahau milele, pamoja na juhudi za wengine kuwaeleza kinyume cha hayo”.
Endelea kusoma habari hii.....................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits