Friday, October 7, 2011

Wanawake watatu washinda tuzo ya Nobel

Best Blogger Tips
Bi Tawakul Karman, Rais Ellen Johnson Sirleaf na Bi Leymah Gbowee
Tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka huu imewatunuku kwa pamoja wanawake watatu- Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, Leymah Gbowee wa Liberia na Tawakul Karman wa Yemen. 

Wametambulika kutokana na "harakati zao bila kutumia vurugu kwa usalama wa wanawake na haki za wanawake katika kushiriki kikamilifu kwenye kujenga amani".

Bi Sirleaf ni rais wa kwanza mwanamke barani Afrika, Bi Gbowee mwanaharakati wa amani Liberia na Bi Karman kiongozi wa harakati za kidemokrasia Yemen.

Tuzo hiyo ikitangazwa Oslo, mwenyekiti wa kamati ya Nobel Thorbjorn Jagland alisema: " Hatuwezi kufanikiwa kupata demokrasia na amani ya kudumu katika dunia hii mpaka wanawake wafanikiwe kupata fursa sawa na wanaume ili kuweza kuchochea maendeleo katika viwango vyote vya jamii."

Taarifa hiyo ilisema "ni matumaini ya kamati ya Nobel ya Norway kuwa tuzo hiyo itasaidia kumaliza ukandamizaji wa wanawake ambao bado unaendelea katika nchi nyingi, na kutambua uwezo mkubwa wa demokrasia na amani ambao wanawake wanaweza kuwakilisha."

'Mwanamke Ngangari'

Bi Karman anaongoza shirika la Yemen la Women Journalists without Chains, yaani waandishi wa habari wa kike wasio na mipaka na amefungwa jela mara nyingi kutokana na kampeni zake za kutaka uhuru wa habari na upinzani wake kwa rais wa serikali ya Ali Abdullah Saleh.

Alitambuliwa kwa kuchukua nafasi kubwa kwenye harakati za haki za wanawake katika machafuko ya kuunga mkono demokrasia huko Yemen "katika hali ngumu sana".

Bi Karman, mama mwenye watoto watatu, ameiambia idhaa ya Kiarabu ya BBC kuwa anatunukia tuzo yake kwa "wote waliojitoa mhanga na kujeruhiwa na machafuko ya nchi za kiarabu"- wimbi la ghasia lililoenea Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita na kwa " watu wote wanaopigania haki zao na uhuru wao".

Ni mwanamke wa kwanza wa kiarabu kushinda tuzo ya amani ya Nobel.
Bw Jagland amesema ukandamizwaji wa wanawake ndilo "jambo muhimu sana" katika dunia ya kiarabu na kumtunukia Bi Karman ni "kutoa ishara kwamba kama itafanikiwa katika jitihada za kuleta demokrasia, lazima iwahusishe wanawake".

Bi Sirleaf, mwenye umri wa miaka 72, ambaye tetesi kwa kiasi kikubwa zilikuwa zikimwelekeza yeye, alisema tuzo hiyo ni " kwa Waliberia wote" na kutambuliwa kwa " miaka mingi ya harakati za kupata haki".

Alichaguliwa mwaka 2005, kufuatia kumalizika kwa miaka 14 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 250,000, na kusababisha wengi kukimbilia nchi za nje na kuvuruga uchumi wa nchi hiyo.

Alipoingia madarakani, mchumi aliyepata elimu yake Marekani na aliyekuwa waziri wa fedha- anayejulikana kama "mwanamke Ngagari" wa Liberia aliahidi kupambana na rushwa na kuleta "hisia za kimama kwenye urais" kama njia ya kuponyesha majeraha yaliyotokana na vita.

Ni maarufu sana miongoni mwa wanawake na wasomi wachache nchini humo, lakini anachukiwa na jamii za kimila zinazoongozwa zaidi na wanaume.

Bi Sirleaf anagombea tena urais wiki ijayo, licha ya kusema kuwa atashikilia nafasi hiyo ya urais kwa mhula mmoja tu.

Bi Gbowee alikuwa kinara wa kupinga vurugu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe Liberia, akiwashawishi wanawake wa makabila na dini zote katika harakati za amani- wakati fulani hata "kugoma kufanya ngono"- na kuwahimiza kushiriki kwenye uchaguzi.

Taarifa kuhusu tuzo hiyo ilisema, " Tangu wakati huo amaefanya kazi ya kuwashawishi wanawake Afrika Magharibi wakati na baada ya vita."

Wanawake hao watagawana zawadi yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 1.5.
Chanzo: BBC

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits