Wednesday, October 19, 2011

Hotuba ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kwa Waandishi wa habari Monduli, Octoba 19, 2011

Best Blogger Tips

NDUGU wana habari nimewaita katika mkutano huu leo kwa sababu moja kubwa, kutoa ufafanuzi kuhusu matukio ambayo yamekuwa yakitokea huku yakinihusisha mimi binafsi kwa namna ambayo sasa yanatishia ustawi na mshikamano wa kimaadili, kihistoria na kikazi miongoni mwa viongozi na baina ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

"Ndugu wana habari, naamini mmekuwa mkifuatilia kwa karibu habari zinazoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari zinazolihusisha jina langu na harakati kadha wa kadha chafu ambazo hata mimi mwenyewe ninayehusishwa nazo huwa nazisikia na kuzijua baada ya kuwa zimesharipotiwa katika vyombo hivyo vya habari," alisema.

Alisisitiza kwamba uamuzi wake wa kukutana wanahabari haukuwa na nia ya kuzozana na vyombo vya habari wala kwenda kinyume cha utamaduni wa kimaadili wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) unaotaka viongozi kujadili masuala yanayokihusu chama chao ndani ya vikao rasmi vya kimaamuzi, bali kutoa ufafanuzi na angalizo kwa pande zote hizo mbili ambazo zinaguswa na matukio yanayoendelea kutokea.

Moja ya mambo ambayo yameligusa jina langu kwa namna hiyo ni lile linalonihusisha eti na kundi moja la wanasiasa ambao wamekuwa na mikakati ya kumhujumu mwenyekiti wetu wa chama, Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete. Hakuna shaka ni madai ya kipuuzi, kizushi na yenye malengo machafu.
Hawakuishia hapo sasa wamefikia hatua ya kuvitumia vyombo hivyo hivyo vya habari na kufikia hatua ya kudai kwamba nimeanza kuandaa orodha ya kile wanachokiita madhambi ya Rais Kikwete ambayo wanadai nimepanga kuyasoma wakati wa kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (CCM).

Ninaamini kwa dhati kabisa kwamba, waandishi wa habari wanaofuatilia kwa karibu na kwa umakini mwenendo wa masuala ya kisiasa nchini wanatambua kwamba, watu wanaopenyeza taarifa hizi katika vyombo vya habari wanafanya hivyo kwa malengo ya kufikirika ya kujisafishia njia kisiasa.

Ni jambo lisiloingia akilini kunihusisha na kile kinachoitwa mikakati ya kumhujumu rais au chama ambacho mimi ni kada wake wa muda mrefu, mbunge anayetokana na chama hicho hicho na mtu ninayeiongoza Kamati nyeti ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na zaidi ya yote kiongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa na kiserikali nilizowahi kushikilia.

Kuhusu hili napenda kusema kwa uwazi kwamba, mbali ya ukweli kuwa sijapata kufikiria hata mara moja kuhusu hicho wanachokiiita mabaya au madhambi ya rais, sina na wala siijui hiyo wanayoitaja kuwa ni orodha ya mabaya ya namna yoyote dhidi ya Rais Kikwete.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits