Saturday, October 8, 2011

Wabrazil waahidi kuitoa nchi gizani

Best Blogger Tips
MATUMAINI ya Watanzania kuwa na umeme wa uhakika, yameanza kuonesha nuru, baada ya Ijumaa, kampuni ya Odebreicht ya hapa kukubali kuwekeza katika umeme wa maji kwenye maporomoko ya maji ya Stiglers Gorge yaliyopo ndani ya Bonde la mto Rufiji, umbali wa kilomita 374 kutoka jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ilifikiwa Ijumaa katika mazungumzo kati ya wawakilishi wa kampuni hiyo kubwa ya uwekezaji katika sekta hiyo duniani kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo jijini hapa, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja alisema mradi huo utakaoanzishwa katika Bonde la Rufiji, ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 2,100.

Mahitaji ya nchi hayazidi megawati 1,000 ingawa kwa sasa umeme unaozalishwa kutoka
mitambo ya vyanzo vya maji na mafuta unafikia megawati 500, hivyo kufanya upungufu wa kati ya megawati 300 na 500 ambazo zikipatikana zitaiondoa kabisa nchi gizani.

Hivyo, kupatikana kwa umeme wa Brazil kutakuwa kumeandika historia mpya, kwani tatizo la umeme linaweza lisionekane kwa miaka mingi ijayo.

Alisema kampuni hiyo ilisema imeridhishwa na mradi huo baada ya kutembelea Tanzania
Agosti 17, mwaka huu na kuthibitisha kuwa mradi huo unawezekana.

"Hawa watu wana uwezo mkubwa, kwani huu hautakuwa mradi wao wa kwanza, walishakuwa na mradi kama huo nchini mwao hapa ambao unazalisha megawati 3,150...tunaamini watafanya vizuri," alisema Ngeleja.

Alisema mradi huo ambao umekuwa ukipigiwa kelele muda mrefu na wananchi, ukikamilika utaiwezesha Tanzania kujitosheleza kwa nishati hiyo na kuuza mwingine nje ya nchi na kuipatia nchi fedha za kigeni.

Aliongeza kuwa mbali na kuuza nje, lakini pia utakuwa wa bei nafuu kwa wananchi. Hata hivyo Ngeleja alisema Serikali haitakaa na kubweteka ila itaendelea kutafuta vyanzo zaidi vya umeme ili kuhakikisha kuwa tatizo linalojitokeza hivi sasa la umeme halijirudii.

Aliongeza kuwa licha ya hivyo bado Tanzania haitategemea vyanzo vya umeme wa maji pekee bali itaendelea kutafuta vingine jinsi itakavyowezekana.

Kabla ya kujitokeza kwa mwekezaji huyo wa Kibrazil, serikali ilikuwa katika juhudi za kuendeleza mradi wa Stigler’s Gorge tangu miaka ya 1970, kwa kufanya upembuzi yakinifu kwa msaada wa serikali ya Norway, lakini hakuna uendelezaji wowote uliokuwa umefanyika katika mradi huo wa kufua umeme.

Kuhusu mafuta, alisema Kampuni ya Petrobras ya hapa ambayo ilitoa meli kubwa ya
kutafuta mafuta Tanzania inaendelea na juhudi zake katika mwambao wa Bahari ya Hindi
na mpaka sasa haijapata mafuta wala gesi lakini matarajio ni makubwa.

Alisema Petrobras ambayo pia ni kampuni kubwa ya mafuta nchini hapa inatarajia kutoa taarifa ya awali ifikapo Desemba.

Kuhusu juhudi za Serikali kutafuta wabia wa miradi hii, Ngeleja alisema Serikali inafanya hivyo kwa kuwa haina fedha za kutosha yenyewe kuiendeleza na ndiyo sababu inashirikisha sekta binafsi.
Chanzo: HabariLeo

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits