Thursday, October 20, 2011

Wasifu wa Kanali Muammar Gaddafi

Best Blogger Tips

Kanali Muammar Gaddafi
Alikuwa mtoto wa wafugaji wa Kibedui, mwenye maisha ya utata, lakini ambaye alitukuzwa sana, huku mataifa ya Magharibi yakimuona mtu wa hatari wakati wote.

Muammar Muhammad Gaddafi aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 40. Hadi mwanzoni mwa Machi 2011, alikuwa akiamini ndani ya moyo wake kwamba watu wake walikuwa wakimpenda na kwamba walikuwa tayari kumlinda hadi kufa kwa ajili yake.

Lakini wakati huo, tayari Gaddafi alikuwa ameshatumia njia za kikatili kuyazima maandamano dhidi yake, maandamano ambayo baadaye yaligeuka vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kwa mujibu wa taarifa, watu zaidi ya 30,000 waliuawa kwenye vita hivyo. Mara nyingi sana, Gaddafi alitoa matamko makali wakati wa vita hivyo, ila linalojuilikana zaidi ni lile la kuwaita wapinzani wake kuwa ni panya.

Kwa kila hali, yaliyotokea ni mambo ambayo Gaddafi hakuyatarajia asilani. Mtoto huyu wa wafugaji wa Kibedui aliyezaliwa mwaka 1942, alikuja kuibuka kama mkombozi wa Walibya, alipompindua Mfalme Idriss hapo mwaka 1969.

Kuanzia hapo akaanza kujenga kile alichokiona mwenyewe kuwa ni mfumo wa kidemokrasia wa moja kwa moja. Alianzisha kamati za umma zilizoamua juu ya mustakabali wa umma na wa Serikali. Aliuita mfumo wake wa kisiasa na kiuchumi kuwa ni wa kisoshalisti, alioufafanua kwenye kijitabu chake cha Kijani.

Historia yake kiufupi

Alizaliwa mwaka 1942 katika eneo la Jangwa, kwenye mji wa Sirte, katika familia ya baba Mohamed Abdulsalama Abuminiar na mama Aisha Ben Niran. Alijiunga na Jeshi la Libya  mwaka 1965.
Alifanya mapinduzi ya Serikali yasiyo ya umwagaji damu na kumuondoa mfalme Idris katika utawala wake mwaka 1969 na kuwa mtawala wa Libya akiwa na umri wa miaka 27.

Alikuwa maarufu kwa nguo anazopenda kuvaa na walinzi wa kike wenye kubeba silaha, kiongozi huyo wa Libya pia anadhaniwa kuwa na mbinu nzuri za kisiasa kwa kuweza kuirejesha Libya kutokana na kutengwa kidiplomasia duniani.
Baada ya miongo miwili ya kutengwa katika jamii ya kimataifa, mwaka 2003, Tripoli ilikiri kuwa walifanya shambulio la Lockerbie kwa kuiangamiza kwa mabomu ndege ya Pam Am. Umoja wa Mataifa (UN) ulikubali kuondoa vikwazo dhidi ya Libya.

Baada ya miezi kadhaa, Serikali ya Kanali Gaddafi ilisitisha mipango yake ya kuunda silaha za maangamizi na hii ikarejesha ushirikiano na nchi za Magharibi.

Gaddafi ni mtu wa kipekee katika kauli zake, mienendo yake, tabia zake na mikakati yake, kwa mujibu wa Saas Djebbar, mtaalam wa siasa za Libya.
Alipokuwa kijana alivutiwa na kiongozi mzalendo wa Misri, Gamal Abdel Nasser, alipokuwa akishiriki katika maandamano dhidi ya Israel wakati wa mtafaruku wa Suez mwaka 1956.

Alipanga njama ya kupindua utawala wa kifalme alipokuwa mwanafunzi wa kijeshi alipokuwa mafunzoni Uingereza kabla ya kurejea nyumbani Libya. Alipanga mapinduzi ya Septemba 1, 1969 akiwa katika mji wa Benghazi.

Alianza kujenga itikadi zake za kisiasa mwaka 1970 na kuziandika katika kitabu chake cha kijani kibichi.
Alikitumia kitabu chake kuanzisha mfumo wa kisiasa uliojumuisha kanuni za Kiislamu na mfumo ulio tofauti na siasa za ujamaa au ubepari.
Mwaka1977 aliasisi mfumo ujulikanao kama 'Jamahiriya' au 'Taifa la Umma' ambapo raia ndio wanaoendesha uongozi wa nchi yao kupitia 'kamati za umma'.

Mfumo huo wa Gaddafi umevuka mipaka na hauhusishi mambo ya siasa tu, bali pia mambo mengine.
Akiwa safarini ng'ambo, alikuwa akitumia makazi maalum kwenye kambi iliyojengwa na hema yake ya kifahari ya Kibeduwi akiwa amefuatana na walinzi wanawake ambao, inasemekana, huwa hawapotezi umakini kazini kama walinzi wanaume.Hema hiyo pia ilitumiwa kuwalaki wageni wa Libya na Kanali Gaddafi huendesha mikutano na mahojiano yake humo humo akipepea usinga au tawi la mitende.

Rais wa zamani wa Marekani Ronald Reagan alimwita Gaddafi 'mad dog' yaani 'mbwa kichaa' na Marekani ililipiza kisasi dhidi ya Libya kwa madai ya kuhusika na mashambulio ya anga barani Ulaya kwa kuvamia miji ya Tripoli na Benghazi mwaka 1986.Aliposhindwa katika jitihada zake za kuzipatanisha nchi za Uarabuni katika miaka ya 90, Kanali Gaddafi alielekeza nguvu zake barani Afrika na kupendekeza 'Muungano wa Nchi' za bara la Afrika.

Alianza kuvaa mavazi yake binafsi, sare za michezo zilizo na ngao za Bara la Afrika au picha za viongozi kutoka bara hilo.Aliwahi kuvunja na kufuta Wizara za nchi hiyo pamoja na bajeti zao, isipokuwa Wizara chache ikiwemo ya Ulinzi, Fedha na Mambo ya Nje.Licha ya uchumi wa Libya kutoa fursa kwa wawekezaji wa nje, mabadiliko bado yanakwenda taratibu.

Vuguvugu la mageuzi dhidi yake lilipoanza mwanzoni mwa mwaka huu, aliapa kuwafuata wanaompinga nyumba hadi nyumba, mlango kwa mlango, hatua iliyoibua hasira na kuchochea harakati za kijeshi dhidi yake.

Baada ya baadhi ya askari kutangaza kujitoa katika jeshi lake na kuanzisha uasi, aliapa kwamba atapambana hadi tone la mwisho la damu litakapomwagika. Alisisitiza kwamba kamwe hatakimbia kutoka katika ardhi ya Libya, atafia katika ardhi ya mababu zake.

Taarifa zilieleza jana kwamba aliuawa baada ya kukutwa akiwa amejificha katika daraja dogo kwa ajili ya kupitisha maji barabarani (karavati).
Mara baada ya kuuawa, wapiganaji wa Baraza la Mpito waliokuwa katika mapambano dhidi yake walibaini kwamba alikuwa na bastola iliyotengenezwa kwa dhahabu tupu.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits