Friday, July 27, 2012

Dar katika orodha ya majiji 12 machafu duniani

Best Blogger Tips
 INAKADIRIWA kuwa  Jiji  la Dar es Salaam, linazalisha tani 4,252 za taka kwa siku na kwamba ni kati ya asilimia 26 na 37 tu, zinazozolewa na kutupwa dampo.Hayo yalisemwajana na Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, katika hotuba yake katika warsha kuhusu kubuni mikakati ya kusimamia usafi wa mazingira ya jiji.

Warsha hiyo inawashirikisha wadau mbalimbali wa mazingira.Meya huyo alisema majiji mengi katika nchi zinazoendelea, yana mazingira machafu ikilinganishwa nay ale ya nchi zilizoendelea na kwamba hali hiyo inatokana na  changamoto  nyingi ukiwemo ukomo wa bajeti.

Hali  kadhalika wingi wa watu wanaohamia  mjini na mipangilio mibovu ya miji.Dk Masaburi alisema kwa assa Jiji la Dar es Salaam, linakadiriwa kuwa na wakazi milioni nne na nusu  huku ongezeko la wahamiaji likiwa limefikia asilimia 4.3.

Alisema ongezeko hilo la watu, limesababisha  Jiji hilo kukua kwa kasi kubwa.

“Asilimia 70 ya watu hao wanaishi katika maeneo yasiyopimwa na mimi ni miongoni mwao,” alisema Dk Masaburi.

Alisema ongezeko hilo la watu,  limesababisha mamlaka za halmashauri,  kushindwa kumudu kutoa kwa ufanisi,  huduma za miundombinu ya barabara, afya, majisafi, maji taka na mipango miji .

Alibainisha kuwa Jiji la Dar es Salaam, linakadiriwa kuzalisha wastani wa tani 4,252 za taka kwa siku.
Alisema kwa kuzingatia changamoto hizo, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa kushirikiana na wadau wengine, imeanzisha sehemu ya kutengeneza mbolea ya mboji kwa kutumia takarejea, zinazotokana na mabaki ya vyakula mbalimbali.

Kwa mujibub wa meya, mbolea hiyo ya mboji inahitajika kwa kiwango kikubwa na wakulima wadogo wadogo na itasaidia kuwa sehemu ya vyanzo kwa vikundi vya kijamii vinavyojishulisha na udhibiti wa taka jijini. “Lakini pia itasaidia  kupunguza hewa ya Carbon inayotokana na taka zenye kemikali zinazosababisha madhara kwa binadamu ukiwemo ugonjwa wa kansa,” alisema.

Kaimu  Mkuu wa Idara ya Udhibiti wa Taka katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Membe Protus,  alisema Jiji hilo  ni la tatu barani Afrika linalokua kwa haraka.

Alisema pia ni moja ya  majiji 12 machafu duniani.Alisema halmashauri zinafanya kazi ya kukusanya uchafu  kwa shida kutokana na upungufu wa vifaa, ikiwemo vya  kuteketeza taka hatarishi husasani zile  za hospitali na zenye kemikali.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits