Monday, July 16, 2012

Mkurugenzi TANESCO atikisa

Best Blogger Tips
SIKU moja baada ya Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, William Mhando, na wenzake watatu kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka, siri nzito imefichuka kuwa ni janja za serikali kutaka kuficha udhaifu na uzembe wake katika kuliwezesha shirika hilo.

Mhando na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga na meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun Matambo, walisimamishwa na bodi hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Jeneralai mstaafu, Robert Mboma ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao.

Hata hivyo Tanzania Daima limedokezwa kuwa mkurugenzi huyo ametolewa kafara kutokana na kutokuwa na mahusiano mazuri kiutendaji na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, lakini na vilevile katibu mkuu huyo anatumia udhaifu wa serikali kwa TANESCO kumwadhibu ili kuepusha mjadala mzito wakati hotuba ya bajeti yao itakaposomwa bungeni hivi karibuni.

Inasemekana sababu inayotolewa na Katibu Mkuu ni kwamba Mhando alimdharau kwa kutompa taarifa kabla ya TANESCO kutangaza mgawo wa umeme wa hivi karibuni. Kwa mantiki hiyo, akamlima Mhando barua akisema anahujumu shirika. Hata hivyo, wananchi na watumishi wa TANESCO wanajua kuwa anayehujumu TANESCO ni serikali, ambayo inalinyima shirika hilo pesa ilizoahidi kwa ajili ya miradi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme, na kulizuia shirika hilo kuuza umeme kwa faida, kwa sababu za kisiasa.

Inasemekana hatua dhidi ya Mhando inatokana na woga wa waziri na katibu mkuu juu ya mjadala mkali unaotarajiwa kuibuka bungeni wakati wa kujadili bajeti ya wizara yao. Mhando anatolewa kafara kisiasa, lakini taarifa zinasema naye amejibu barua ya katibu mkuu kueleza jinsi asivyohujumu shirika hilo. Habari zaidi baadaye.

Katika barua ya Maswi kwa Mhando yenye Kumb.Na. SAB. 270/ 286/01/2 ya Julai 12, mwaka huu, anasema: “Nimesikitishwa na kitendo chako cha kuanza mgawo wa umeme bila kupata kibali cha maandishi kutoka kwangu kama nilivyokueleza katika barua yangu niliyoambatanisha.”

Maswi anaongeza: “Hiyo siyo tu ni dharau bali inaonyesha kuwa mgawo huo wa umeme unafanywa kwa makusudi kwa lengo la kuihujumu serikali. Aidha, ukiwa kama kiongozi mkuu wa shirika, unaonekana umeshindwa kutekeleza majukumu yako ya kusimamia shughuli za shirika inavyostahili.
“Kwa barua hii unipe maelezo kwa nini uliamua mwenyewe kuanza mgawo wa umeme bila kunifahamisha kama inavyotarajiwa, kwa makusudi kabisa uliamua kuanzisha mgawo mikoa yote bila sababu ya msingi ilhali ukijua ni wakati wa Bunge na ili serikali ishambuliwe,” ilisomeka barua hiyo.

Hata hivyo, katika barua yake ya utetezi Mhando anakataa kuhusika na hujuma huku akieleza bayana kile kilichotokea hadi kusababisha mgawo na kwamba hata Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi alipewa taarifa juu ya tatizo hilo.

“Taarifa hii nilimpa pia mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika. Hali hii ilijitokeza kutokana na ukweli kwamba vituo vya kuzalisha umeme vya IPTL na Symbion Dodoma havikuwa na mafuta ya kutosha kuzalisha umeme, na vile vile kulikuwa na upungufu wa gesi asili katika vito vya TANESCO,” alisema Mhando katika barua yake.

Anakataa kuwa hajashindwa kufanya kazi yake hiyo licha ya kuifanya kwenye mazingira yenye changamoto kubwa. “Serikali ingeidhamini TANESCO kupata mkopo wa sh bilioni 408 mapema iwezekanavyo, kuondoa kodi kwenye mafuta yanayotumika kufua umeme na kupata ruzuku ya sh bilioni 80 toka serikalini ifikapo Julai mwaka huu matatizo ya umeme yangelikuwa historia!”

Mhando anaweka wazi kuwa mkopo huo wa sh bilioni 408 ambao ulitegemewa kupatikana mapema tangu mwishoni mwa 2011 mpaka sasa haujapatikana kutokana na ucheleweshaji wa dhamana ya serikali na msamaha wa kodi kwenye mafuta yanayotumika kufua umeme pamoja na ruzuku ya sh bilioni 80 toka serikalini haijapatikana kama ilivyoahidiwa.

Ni katika mazingira hayo wadadisi wa mambo wanaona kama serikali inataka kufunika kombe la kushindwa kutimiza wajibu wake kwa shirika hilo na hivyo kumbebesha lawama Mahando ili isiadhibiwe na wabunge.

Kufuatia utata huo wa kusimamishwa kwa vigogo hao, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Kabwe Zitto, aliliambia gazeti hili jana kuwa wameita kikao cha kamati na kuiita bodi ya TANESCO ili ijieleze na vile vile watakuwepo Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovic Uttoh na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma (PPRA).

“Nitatoa taarifa baada ya kikao. Tunataka uwajibikaji lakini hatutaki uonevu, nimeagiza mwenyekiti wa bodi ya TANESCO aje kujieleza kwenye kamati kuhusu tuhuma hizo,” alisema Zitto.

Naye waziri kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, alisema kuwa kusimamishwa kwa Mhando na watendaji wengine wa shirika hilo ni mbinu ya serikali ya kuficha udhaifu na uzembe unaoikabili.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema hali hiyo inachagizwa na suala zima la ufisadi hali inayotishia nchi kurudi katika mgawo wa umeme kama inavyodhihirika hivi sasa.

Alisema taarifa za utendaji wa TANESCO kuhusu mpango wa dharura wa umeme zimekuwa zikijadiliwa mara kwa mara kwenye vikao vya wizara hiyo hata baraza la mawaziri bila kuchukuliwa hatua muafaka.

“Hii ni kauli rasmi kama waziri kivuli kitendo cha kumsimamisha Mhando na wenzake ni kumtoa kafara ya kuficha udhaifu na uzembe wa serikali juu ya tishio hili la nchi kurejea katika mgawo,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Aliitaka serikali kutoa kauli ya kwa nini waziri na naibu wake walitoa taarifa potofu bungeni kuwa hakuna tishio la mgawo wa umeme, na juu ya mkakati wao aliouita ni dhaifu waliokuwa wakiufanya kupunguza mgawo katika kipindi cha Bunge ili kuficha udhaifu na uzembe uliokithiri.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits