Tuesday, July 31, 2012

‘Dawa ya Babu wa Loliondo ni feki’

Best Blogger Tips
 Utafiti umebaini kwamba dawa iliyokuwa ikitolewa na mchungaji mstaafu Ambilikile Masapila maarufu kama babu wa Loliondo ni feki na kwamba haina uwezo wa kutibu Ukimwi wala kisukari.

Hayo yalielezwa bungeni jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2012/13.

Alisema utafiti wa kulinganisha wagonjwa wa ukimwi na kisukari waliokunywa dawa hiyo na wale ambao hawakunywa umebaini kwamba hakuna utofauti wa afya ya mgonjwa.

Alisema utafiti huo unafanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI), ulianza Machi mwaka huu na kwamba unahusisha wagonjwa 200 wanaofuatiliwa kwa kupimwa damu, kinga ya mwili (CD4) na uzito wa mgonjwa, ambao ulifanyika tangu mgonjwa alipokunywa kikombe cha babu.

“Matokeo ya awali ya utafiti yameonyesha kuwa hakuna utofauti katika vipimo vya kimaabara pamoja na damu, CD4, uzito na ubora wa afya ya wagonjwa kati ya waliokunywa na wale ambao hawakunywa dawa ya mchungaji,” alisema Dk. Mwinyi.

Alisema lengo la utafiti huo ni kubaini uwezo wa dawa hiyo katika kutibu magonjwa aliyosema dawa yake inayatibu ili kuona kama kuna utofauti wowote baada ya mgonjwa kutumia dawa.

Chanzo: Ippmedia

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits