Sunday, July 1, 2012

Dk. Ulimboka aitesa serikali

Best Blogger Tips
 SIKU chache baada ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, kudaiwa kuhusika kwenye sakata la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, imeelezwa kuwa ofisa huyo amewekewa ulinzi mkali.

Habari za ndani ya jeshi hilo zinasema kuwa ofisa huyo anaishi kwa mashaka kutokana na tuhuma nzito aliyotupiwa, hatua iliyowafanya wakuu wake kumpa walinzi wawili wa kulinda usalama wake wakati huu ambapo uchunguzi unaendelea chini ya tume maalumu iliyoundwa.

“Issue ya Dk. Ulimboka imemweka pabaya afande Msangi, anaishi kwa hofu sana hadi kufikia hatua ya kupewa walinzi wawili,” kilieleza chanzo chetu cha habari.

Hata hivyo, pamoja na kukiri kusikia tuhuma hizo ambazo amezikana, Msangi ameliambia Tanzania Daima kuwa, yeye hana hofu kwa kuwa anajua hajafanya wala kuhusika kwa namna moja ama nyingine na tukio la Ulimboka.

Alikanusha kupewa ulinzi, ingawa Tanzania Daima lilishuhudia kwa siku mbili akiwa ameambatana na watu wengine wawili kila alipokwenda, ingawa alikiri kuwa ni askari wake na kwamba hilo ni jambo la kawaida.

Kwa mujibu wa kanuni za kazi za polisi, Kamanda wa Polisi wa mkoa ama wa Kanda Maalumu ndiye tu anayepewa ulinzi binafsi, lakini si mkuu wa upelelezi wa mkoa.

JK, serikali imtese Ulimboka kwa lipi?

Rais Jakaya Kikwete, ameeleza kushangazwa kwake na tuhuma zilizotolewa na baadhi ya madaktari na wana harakati kwamba serikali inahusika kumteka na kumpiga kikatili mwenyekiti wa jumuiya ya madaktari, Steven Ulimboka.

Katika hotuba yake jana kwa Watanzania, Kikwete pamoja na kuelezea masikitiko yake makubwa na kuhuzunishwa na kitendo cha kinyama alichofanyiwa Dk. Steven Ulimboka usiku wa Juni, 26, 2012, alidai kushangazwa na tuhuma kwamba serikali inahusika na ukatili huo, akisema haoni sababu ya msingi ya kufanya hivyo, ikizingatiwa kuwa ndiye aliyekuwa kiungo muhimu baina ya serikali na madaktari.

Kikwete alisema ingawa ni ukweli kwamba Dk. Ulimboka hakuwa mtumishi wa serikali, hivyo hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano hayo na pia kulikuwa na rai ya kutaka asiwepo, bado ndiye aliyeamuru aachwe aendelee kuwapo maadam madaktari wenzake wamemuamini na anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na serikali.

Aliongeza kuwa kutokana na mwenendo wa mazungumzo ulivyokuwa ukiendelea, hakukuwa na sababu za serikali kufikia hatua ya kumdhuru Dk. Ulimboka.

“Kwa nini serikali imdhuru Dk. Ulimboka? Nimeelekeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane. Nimesema kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits