Monday, July 16, 2012

Waziri atishiwa kuuawa

Best Blogger Tips
 WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Terezya Huvisa, amesema ametishiwa kuuawa endapo ataendelea na zoezi la kubomoa nyumba za watu zilizo kwenye maeneo oevu.
Madai hayo aliyatoa jana mjini hapa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema amepigiwa simu za vitisho hivyo kwa lengo la kukwamisha jitihada zake za kuwashughulikia wanaovunja sheria.

Alisema baada ya kupata vitisho hivyo, aliamua kuwapigia simu lakini simu hizo hazikupatikana jambo lililomfanya kuvipuuzia vitisho hivyo.

“Sijaviripoti polisi vitisho, najua lengo lao lilikuwa kunitisha ili nisiendelee na mkakati wa kuwabomolea nyumba wale waliojenga kwa kukiuka sheria, wanajidanganya nitaendelea kuwabomolea,” alisema.

Alisema mtu yeyote mwenye jambo lenye tija na masilahi kwa taifa kamwe asingesita kumpigia simu na ikiwezekana kwenda kumuona juu ya bomoabomoa lakini waliompa vitisho hivyo ni ‘feki’.

Waziri huyo aliongeza kuwa Mwanasheria la Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (NEMC), Heche Manchare, naye alipewa vitisho pamoja na kupigwa na watu waliokuwa wamevalia vitambaa usoni kwa lengo la kuficha sura zao.

Alibainisha kuwa tukio hilo waliripoti kwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, ambaye aliwaambia walifikishe polisi lifanyiwe uchunguzi zaidi.

Aliongeza kuwa pamoja na vitisho hivyo kamwe wizara yake haitarudi nyuma katika zoezi la kuwabomolea nyumba, hoteli au wawekezaji wowote wale waliojenga kwenye maeneo oevu.

“Hili ni zoezi gumu sana linalohitaji ujasiri na umakini mkubwa sana, sisi hatutamuonea mtu yeyote, tumedhamiria kufanya kazi zetu kwa nguvu hatarudi nyuma,” alisema.

Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani, Emanuel Nchimbi, aliwataka viongozi na wananchi wote wanaopata vitisho kuwasiliana na polisi ili hatua zichukuliwe.

Katika hatua nyingine, serikali imeeleza kupata hasara ya sh bilioni 50 kwenye utekelezaji wa zoezi la bomoabomoa katika fukwe za kawe na mbezi jijini Dar es Salaam.

Waziri Huvisa, alisema kuwa kiasi hicho cha fedha ambacho serikali imekitumia ni kikubwa sana na kitalipwa na wamiliki wa nyumba hizo ambao walijenga kinyume cha sheria na watazigawanya kwa viwango mbalimbali kutokana na kila nyumba ilipokuwa imefikia.

Alisema kuwa wizaya yake ilishirikiana na Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Manispaa ya Kinondoni ambapo jumla ya nyumba saba na uzio nane zilibomolewa na ujenzi uliokuwa unaendelea kwenye mkondo wa mto umebomolewa.

Alisema kuwa ubomoaji huu ni utekelezaji wa sheria ya mwaka 2004 kutokana na wananchi hao kukaidi na kutokutekelezwa kwa maagizo mbalimbali ya kutoendelea na ujenzi yaliyotolewa kwa wahusika.

“Nawataka wale wote waliojenga na wanaoendelea kujenga kwenye vyanzo vya maji, kando kando ya bahari, maziwa, mito na mabwawa na misitu inayolindwa kisheria kuondoka mara moja na endapo watakiuka maagizo hayo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao,” alisema waziri huyo.

Alifafanua kuwa hatua zitakazochukuliwa dhidi yao moja wapo ni kuwabomolea nyumba zao na kuwaondoa katika maeneo hayo na kwamba watatakiwa kulipia gharama zote zitakazohusu ubomoji huo.

Waziri alisema kuwa agizo hilo pia linawahusu wakulima na wafugaji wanaofanya shughuli zao katika vyanzo vya maji.
Chanzo: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits