Thursday, July 19, 2012

Uchina kutoa dola bilioni 20 kwa Afrika

Best Blogger Tips
Rais Hu Jintao
 Rais Hu Jintao, Uchina ameziahidi serikali za Afrika mkopo karibu dola za Marekani bilioni 20 kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Amesema kuwa mkopo huo utasaidia katika ujenzi wa miundo mbinu, kilimo na maendeleo ya biashara.

Rais Jintao aliyasema hayo wakati wa mkutano wa ushirikiano baina ya Uchina na viongozi wa Afrika mjini Beijing.

Kuanzia barabara mpya za mjini Nairobi hadi wauza kuku katika soko la Zambia ni dhahiri kwamba Uchina imeweka nyayo zake katika kuinua uchumi wa Mataifa mengi barani Afrika.

Miundo mbinu ni mojawapo ya sehemu ambazo Uchina imewekeza vilivyo barani Afrika.

Biashara kati ya Bara Afrika na Uchina imeongezeka kutoka dola bilioni 10 miaka kumi iliyopita na kufikia takriban dola bilioni mia moja na sitini hii leo.

Nchi hiyo imetoa mikopo zaidi kuliko Benki ya Dunia.

Baadhi ya viongozi wa mataifa ya Afrika wamefurahia uhusiano huu wakisema kuwa utakomesha tabia na hali ya kukaliwa na Mataifa ya magharibi kiuchumi na kisiasa kwa masharti yanayoambatana na mikopo hiyo.

Kwa upande mwingine Uchina imeshutumiwa na nchi za magharibi kama yenye tamaa, hali inayoifanya kupuuza haki za utu na kupendelea maendeleo ya kiuchumi na mahitaji yake ya nishati.
Mataifa ya magharibi hayajasita kuinyooshea kidole Uchina kama Mkoloni mpya wa Afrika, kwa kutangaza rekodi yake ya ukiukaji wa haki za binadamu kwa kisingizio cha kuitojiingiza katika masuala ya ndani ya nchi wanakoendesha shughuli zao.

Mfano uliopo ni nchini Sudan ambako mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekosoa uhusiano na Uchina, licha ya vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea huko Darfur.

Mashirika hayo yanaongezea kusema kuwa Uchina imesaidia katika kuchochea ghasia kupitia msaada wake wa fedha, silaha na sera.

Kwa upande wake Uchina imesisitiza kuwa itaendelea na sera yake ya kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine.

Mpango wa Uchina kwa Afrika ni bayana. Ina hamu ya maliasili kutoka Bara hilo pamoja na soko la bidhaa zinazotengenezwa Uchina. Vilevile, Uchina inataka kudhibiti ushawishi wake wa kibalozi ulimwenguni kwa msaada wa Afrika.

Hivyo ndivyo hali ilivyo kuhusu miradi ya Uchina kwa Afrika ambapo watu wengi hudhani kuwa Uchina ndiyo inayodhamini miradi yote.

Benki ya Maendeleo ya Afrika, ADB huenda ikahisi kuwa Wachina wameipokonya hadhi yake kutokana na kwamba watu wengi wanaonelea hata miradi ya Benki hiyo na kudhani imedhaminiwa na Wachina, ingawaje fedha zimetoka kwenye Benki hiyo lakini wahandisi na wajenzi ni Wachina.

Viongozi wa Kiafrika hukumbushwa kuhusu mshirika wao mpya wanapokwenda Addis Ababa kwenye makao makuu ya Umoja wa Afrika.

Jengo kabambe la kisasa lililojengwa kwa vioo na mawe kwa gharama ya dola milioni 200 lilidhaminiwa na Uchina, bila shaka.
Chanzo: BBC

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits