Sunday, July 1, 2012

Hotuba ya Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete, June 30, 2012

Best Blogger Tips
 Ndugu Wananchi,

Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma, kwa kutujaalia uzima na kutuwezesha kumaliza nusu ya kwanza ya mwaka 2012 salama.  Kwa kutumia utaratibu wetu wa kuzungumza nanyi kila mwisho wa mwezi, leo napenda kuzungumzia mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la usafirishaji haramu wa binadamu nchini na la pili ni la mgomo wa madaktari.  
Usafirishaji Haramu wa Binadamu Nchini

Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mtakuwa mmezisikia taarifa za tukio la kushtusha na kuhuzunisha la kukutwa maiti 43 za watu wasiojulikana, zilizotupwa katika kichaka kilichopo kijiji cha Chitego, Wilayani Kongwa, Mkoa wa Dodoma tarehe 26 Juni, 2012.  Pamoja na maiti hao, walipatikana watu 84 wakiwa hai lakini wote wakiwa wamedhoofu na baadhi yao wakiwa mahututi. 

 Hatua za haraka zilichukuliwa kuwasafirisha watu hao hadi Dodoma ambapo wale waliokuwa mahututi walifikishwa Hospitali Kuu ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu na wengine walihifadhiwa katika Kituo cha Kati cha Polisi, Dodoma.  Maiti 22 zilipelekwa Dodoma na 21 zilipelekwa Morogoro kuhifadhiwa.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa wale walionusurika zimebainisha kuwa watu hao ni raia wa Ethiopia ambao walikuwa safarini kwenda Malawi na baadaye Afrika ya Kusini ambako wangetengenezewa utaratibu wa kwenda kuishi Marekani na Ulaya. 
 Kwa mujibu wa maelezo yao, safari yao ilianza miezi mitano iliyopita.  Mwezi mmoja waliutumia Ethiopia na miezi minne waliitumia Kenya kabla ya kuletwa Arusha ambako walipakiwa kwenye lori na kuanza safari ya kuelekea Malawi lakini ikaishia Chitego.  Lori walilopanda lilikuwa limezibwa kabisa na hivyo kusababisha vifo kwa kukosa hewa.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits