Monday, July 16, 2012

Wabunge wote vijana kupigishwa kwata JKT

Best Blogger Tips
 WABUNGE vijana walioko katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watapaswa kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa Mujibu wa Sheria kuanzia mwaka huu wa fedha wa 2012/13.
Waziri wa Ulinzi na JKT, Shamsi Vuai Nahodha alisema hayo alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya wizara yake bungeni jana. Alisema wabunge vijana watakuwa sehemu ya kundi la kwanza la vijana 5,000 katika mafunzo yatakayoanza Machi, mwakani.

Alisema wizara hiyo imelifanyia kazi ombi la kuandaa mafunzo ya JKT kwa wabunge vijana kama ilivyoombwa mwaka jana na kwamba wabunge hao wameandaliwa mafunzo hayo ya wiki tatu.
“Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Wizara yangu imelifanyia kazi ombi hilo na kuandaa utaratibu wa mafunzo maalumu ya wiki tatu kwa waheshimiwa wabunge vijana,” alisema Nahodha na kuongeza:

“Kwa hiyo wabunge vijana wataungana na kundi la kwanza la vijana 5,000 niliowaeleza hapo juu… naomba waheshimiwa wabunge mjiorodheshe kwa maandalizi ya mafunzo haya.”
Waziri Nahodha alisema ni imani yake kuwa, pamoja na wabunge kunufaika na mafunzo hayo, watahamasisha urejeshwaji wa mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria na kutoa taswira nzuri ya mafunzo hayo kwa jamii.

Alisema JKT tayari imefanya maandalizi ya kutosha na kwamba kambi tano zenye uwezo wa kuchukua vijana 20,000 kwa wakati mmoja zimeshaandaliwa kwa ajili hiyo.
Alizitaja kambi hizo kuwa ni Bulombora na Kanembwa za mkoani Kigoma, Mlale ya Ruvuma, Msange mkoani Tabora na Oljoro hukoArusha.

Hata hivyo, alisema gharama ya kuendesha mafunzo hayo ni kubwa hivyo JKT haitaweza kuchukua vijana wote na ndiyo maana imeamua kuanza na hao 5,000.
“Vijana hao ni miongoni mwa vijana 41,348 ambao watahitimu mafunzo ya kidato cha sita katika mwaka 2013,” alisema Nahodha.

Kuhusu utaratibu wa kujiunga na kambi hizo, Nahodha alisema uandikishaji wa vijana shuleni utafanyika kati ya Desemba mwaka huu na Januari 2013 na kwamba kambi zitawapokea kati ya Machi 7 na 16, mwakani.Alisema mafunzo hayo ya miezi sita yataanza Machi 17 mwakani na kuendelea hadi Agosti 16.

Wanajeshi Syria

Katika hatua nyingine, Nahodha alisema wanajeshi wa Tanzania kati ya 100 na 200 wanatarajiwa kwenda Syria kuwa waangalizi wa amani ikiwa ni kuitikia ombi la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa Serikali.

Alisema ombi hilo linatokana na utendaji mzuri wa jeshi hilo na kwamba tayari Serikali imelikubali.
Nahodha alisema tayari Makao Makuu ya Jeshi yameanza maandalizi ya kuwapeleka waangalizi hao.
Alisema Tanzania ina wajibu wa kushirikiana na nchi nyingine kulinda amani duniani na imekuwa ikishiriki katika operesheni mbalimbali za kulinda amani.

Katika hatua nyingine; Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Christowaja Mtinda alilalamikia kitendo cha Wahindi kuuza bidhaa za maduka ya jeshi kwa gharama za juu, wakati bidhaa hizo hazilipiwi kodi.
Alisema ni lazima Serikali ieleze Wahindi hao wanauzaje bidhaa za kwenye maduka ya jeshi kwa gharama kubwa wakati maduka hayo yanatakiwa yauze bidhaa hizo kwa bei ya chini.

“Ukienda sasa hivi wanauza sukari Sh1,800 wakati nje ya maduka hayo sukari kilo ni Sh2,000, hili haliwezekani. Wanauza friji, tv kwa bei ya juu na TRA, maofisa wa jeshi wa ngazi za juu wote wanajua,” alisema.

Mtinda alitaka suala hilo litafutiwe ufumbuzi ili bidhaa ziuzwe kwa bei inayotakiwa. Pia alilalamikia nyumba za maofisa wa jeshi akisema haziridhishi na kwamba zinahitaji kukarabatiwa upya.

“Nyumba za maofisa wa jeshi zinatia aibu, hazijakarabatiwa kitu ambacho kinasababisha wafanye ukarabati kwa fedha zao wenyewe,” alisema.

Wapinzani wang’aka

Kwa upande wake, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu wizara hiyo, Mchungaji Israel Natse aliitaka Serikali kutoa maelezo ya matumizi ya Sh4.048 bilioni ambazo zilitumika kuondoa matrekta bandarini.
“Hakika fedha hizi ni nyingi sana kwa kazi ya kuondoa tu matrekta bandarini, Kambi ya Upinzani inataka kupata majibu ni matrekta mangapi yaliondolewa na gharama ya kuondoa trekta moja ilikuwa kiasi gani?” alisema Natse alipokuwa akitoa maoni ya kambi hiyo.

Natse ambaye pia ni Mbunge wa Karatu (Chadema) alisema malipo hayo yanatia shaka na kwamba Serikali lazima ieleze fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi gani.
Kuhusu migogoro ya ardhi, mbunge huyo alisema kumekuwapo na migogoro kwa muda mrefu baina ya wanajeshi na wananchi kwenye maeneo mbalimbali ya nchini na kwamba ni kama hakuna dalili kwamba kuna nia ya dhati ya kumalizwa kwa matatizo hayo.

“Migogoro hii imesababisha kuwapo kwa mvutano baina ya wananchi na jeshi letu kwa upande mmoja na viongozi wa wananchi kwa upande wa pili,” alisema Natse.
Alitoa mfano wa maeneo hayo kuwa ni Ilemela, Tarime, Kunduchi na mengine mbalimbali ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wabunge kwa muda mrefu.

“Mara zote Serikali imekuwa ikitoa majibu kuwa itawalipa fidia wananchi ili waweze kuondoka na kuyapisha maeneo hayo kwa ajili ya jeshi, kwa mwaka huu wa fedha 2012/13 zimeombwa kiasi cha Sh1 bilioni kwa ajili ya kulipa fidia ya ardhi maeneo ya Mapinga, Shinyanga na Arusha.”
Alisema kutokana na fedha hizo ni dhahiri kwamba hakuna nia ya dhati ya kumaliza migogoro baina ya jeshi na wananchi kwani kiasi hicho kilichotengwa ni kidogo na ni kwa ajili ya kulipa fidia na sehemu chache tu.

“Tunaitaka Serikali iwe na nia ya dhati ya kuwalipa wananchi fidia ili kumaliza migogoro hii ambayo inawafanya wananchi walichukie jeshi lao,” alisema.
Chanzo: Mwananchi

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits