Thursday, July 7, 2011

Biashara zafungwa Uganda siku ya pili

Best Blogger Tips
Via BBC

Wafanya biashara katika mji mkuu wa Uganda, Kampala wamefunga maduka yao kwa siku ya pili mfululizo kulalamikia kiwango cha sarafu ya nchi hiyo kinachoshuka kila kukicha pamoja na idadi kubwa ya wachuuzi wenye asili ya Kichina.

Wauza maduka wanadai kuwa sarafu dhaifu inapandisha bei za bidhaa kutoka nje.

Wakati huo huo wanasema hawawezi kushindana na wafanya biashara wa Kichina waliomimina bidhaa zao kwa wingi na kwa bei rahisi.

Mgomo wao wa siku mbili ni tukio la hivi sasa katika mfululizo wa maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama za maisha nchini Uganda.

Polisi wa kuzuia fujo walikuwa mitaani kulinda doria katika mji wa Kampala, kuzuia uwezekano wa kuzuka ghasia.

Msemaji wa shirika la wafanyabiashara la jiji la Kampala, Issa Sekito amesema kua wamefunga maduka yao kuishinikiza serikali ishughulikie masaibu yao.

Bw.Sekito amesema kua shirika lake limeitaka serikali ushughikie biashara za Wachina ambao wamezidsha kujiimarisha nchini Uganda.

Bw.Sekito aliliambia gazeti moja la nchini Uganda kuwa ''Kwa mda sasa,tumekua tukiilalamikia serikali juu ya hawa wageni wanaoshiriki biashara ndogo ndogo,hususan Wachina, wanaokuja wakidai eti ni wawekezaji'.

Shilingi ya Uganda ilidondoka kufikia kiwango cha chini dhidi ya dola ya Marekani mwezi uliopita hadi Benki kuu ilipoingilia kati kujaribu kuiimarisha.

Shirika la habari la Reuters limearifu kuwa 'Mgomo huo umesababisha bei ya bidhaa kama sukari na chumvi kupanda nchini humo''.

Mkaazi mmoja wa mji wa Kampala aliyehojiwa na shirika hilo, Linda Sempijja alisema kuwa maisha yamekuwa magumu kwa sababu bei ya bidhaa zote imepanda.

Mkaazi huyo aliongezea kusema kuwa hawezi kuwalaumu wafanyabiashara, kwa sababu wao pia wanakabiliwa na hali ngumu. Nailaumu serikali, alisema.

Gazeti la kiserikali la New Vision limearifu kuwa Waziri wa Biashara na viwanda,Bi.Amelia Kyambadde alikutana na wafanyabiashara kwa mda wa saa sita.

Waziri huyo aliwasilisha ujumbe kutoka kwa Rais Museveni akiwahimiza wasimamishe mgomo wao, kwa mujibu wa gazeti hilo.

Wafanyabiashara, hata hivyo walisema hawatofungua maduka yao na kwamba mgomo wao utaendelea hata siku ya leo alhamisi.

Wadadisi wanasema kuwa mgomo wao ni ishara ya hivi karibuni inayoonyesha hali ya ongezeko la kutoridhia kwa wananchi kwa serikali ya nchi.

Mnamo mwezi Aprili, vyama vya upinzani vilianzisha maandamano ya kususia usafiri wa umma na kutembea kwenda kazini, kama ishara ya kuitaka serikali itambue ukweli wa kupanda kwa gharama za maisha.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema kuwa vikosi vya usalama viliua watu tisa walioshiriki maandamanao hayo.

Serikali ilivilaumu vikundi vya upinzani kwa kujaribu kuteka madaraka kupitia ghasia baada ya kushindwa katika Uchaguzi mkuu uliofanywa mwezi Febuari.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits