Sunday, July 17, 2011

Sita amkaba koo Ngeleja

Best Blogger Tips
Via Mwananchi

SUALA la mgawo wa umeme unaoendelea nchini kote linazidi kuchukua sura mpya baada ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta kutaka wote waliofikisha nchi kwenye mgawo huo wawajibishwe.
Sitta alisema haitoshi kwa watu hao kuomba msamaha pekee kwa kulingiza taifa katika makali na kadhia ya mgawo huo unaoendelea kuporomosha uchumi wa nchi.


Kauli ya Sitta imekuja wakati wabunge mjini Dodoma wakiwa wamebana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja wakitaka aeleze jinsi atakavyomaliza mgawo huo nchini baada ya kuwasilisha bajeti ya wizara yake juzi, vinginevyo hawataipitisha.

Sitta akizungumza na Vijana wa CCM kutoka vyuo vikuu mkoani Mbeya jana  alisema: “Ni lazima tuwaombe radhi Watanzania kwa kuwapo kwa mgawo wa umeme kwani hii siyo nchi ya kupata mgawo.”

“Tunazo rasilimali nyingi ambazo zinaifanya Tanzania kuwa na umeme wa kuuza na siyo mgawo,” aliongeza Sitta.

“Haitoshi kuwaomba radhi Watanzania lazima waliotufikisha kwenye mgawo wawajibishwe, hili lazima tutalishughulikia tunawaahidi lazima nchi yetu ibaki kuwa na heshima aliyoiacha Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere), ”alisema Sitta.

Sitta ambaye ameongozana na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe (ambaye ni Mbunge wa Kyela), Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela, alisema ili nchi iweze kurejea katika hadhi yake iliyokuwa nayo lazima utaratibu wa kuwajibishana urejewe.

Wengine waliohudhuria kongamano hilo ni Naibu Waziri wa Viwanda Biashara na Masoko ambaye pia ni Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mary Mwanjelwa, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na Mbunge wa Mbarali, Dickson Kilufi.

Katika kongamano hilo pia, Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa alizungumzia jaribio la kutaka kuvuliwa uanachama wa CCM mwaka 2009, akisema kuwa kundi la watu wachache wenye fedha walitaka kutumia fedha zao kumng’oa na kumvua uanachama.

“Nataka kuwaeleza haya matukio yapo ya kutaka kufukuzwa kwenye chama, kwani hata mimi nilitaka kufukuzwa na watu wenye fedha, lakini walishindwa, tunamshukuru Rais Jakaya Kikwete aligundua kuwa kuna ulazima wa kuvua gamba katika chama chetu,”alisema.

“Nawapa matumaini katika chama chetu kuwa sisi mnaotuona hapa ndio tunaotumia akili siyo tumbo katika kufikiri, hivyo chama chetu kitakwenda vizuri,”aliongeza Sitta.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wa Serikali na wanachama wa CCM wanatanguliza ubinafsi, kwani hivi karibuni walidiriki hata kusafirisha wanyama na kuwapeleka nje ya nchi.

“Hivi karibuni kuna wenzetu walisafirisha wanyama wetu aina ya twiga wapatao130 kuwapeleka Uarabuni, hii hali hatutaweza kukubaliana nayo, lazima tupambane,” alisema.

Akijibu maswali ya wanafunzi hao, Sitta alisema kuhusu soko la ajira katika Jumuia ya Afrika Mashariki, vijana wategemee kuwapo kwa ajira hizo na kwamba watapimwa uwezo huku akiwahakikishia kuwa wapo watakaoajiriwa na kufanya kazi Kenya.
Endelea kusoma habari hii.........................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits