Saturday, July 30, 2011

Iringa inaongoza kwa VVU

Best Blogger Tips
Sehemu ya mji wa Iringa
WAZIRI wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda, ameutaja mkoa wa Iringa kuongoza nchini kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Masasi, Mariam Kasembe (CCM), aliyetaka kujua ni mashirika mangapi kutoka nje ambayo yanatoa misaada nchini kwa ajili ya kupambana na janga la ukimwi.

Aidha mbunge huyo alitaka kujua hali ya maambukizi ya virusi vya ukimwi nchini ikoje kwa sasa na takwimu za mikoa ambayo inaongoza na ambayo ina hali nzuri.

Dk. Mponda alisema kuwa kwa sasa mashirika ya nje 16 ndiyo yanayotoa msaada dhiti ya vita ya ukimwi nchini na kwamba mashirika hayo hutoa misaada ya kifedha na kiufundi katika kutekeleza afua mbalimbali zinazolenga kuzuia maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na kutoa huduma kwa wale wanaoishi na VVU.

Alisema baadhi ya afua zinazotolewa ni pamoja na uzuiaji wa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT), huduma ya ushauri nasaha na upimaji wa VVU, kuelimisha jamii katika masuala mbalimbali ya ukimwi.

Alizitaja huduma nyingine kuwa ni pamoja na huduma za kimaabara, matibabu ya magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya ngono, kusambaza kondom na kutoa huduma ya tohara kwa wanaume.

Aidha alisema kuwa ripoti ya tafiti ya viashiria vya VVU na malaria ya mwaka 2008 inaonyesha hali ya maabukizi ya VVU kwa ujumla ni asilimia 5.7 hali ya maambukizi inatofautiana miongoni mwa watu na katika makundi tofauti.

Dk. Mponda alisema kuwa maambukizi yapo zaidi kwa wanawake ambayo ni asilimia 6.8 tofauti na wanaume ambao ni asilimia 4.7, wakati mjini maambukizi ni asilimia 8.7 na vijiji ni asilimia 4.7.

Alisema katika suala la kijiografia mkoa wa Iringa ndio wenye maambukizi ya juu ukiwa na asilimia 14.7 na mikoa yenye maambukizi ya chini ni Kigoma, Arusha, Kilimajaro na Manayara ikiwa na asilimia 2.
Source: Tanzania Daima

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits