Saturday, July 30, 2011

Mbunge aliyeghushi saini ya Pinda abainika

Best Blogger Tips
Jengo la Bunge, Dodoma
Sakata la kughushi saini limeingia katika sura mpya baada Ofisi ya Bunge kumpata Mbunge aliyefanya kitendo hicho na jina lake kukabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Akizungumza na NIPASHE jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema mbunge huyo alipatikana juzi jioni na jina lake lilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu siku hiyo hiyo.

Alisema walilikabidhi jina hilo kwa Waziri Mkuu ili aamue kama atamchukulia hatua ama la na kwamba wamefanya hivyo kwa sababu hakuna mtu aliyelalamikia tukio hilo.

“Hakuna hatua tutakayomchukulia kwa sababu hakuna mtu aliyekuja kulalamikia kwetu na jina la mbunge aliyegushi tumekabidhi kwa Waziri Mkuu ataamua yeye mwenyewe hatua gani atamchukulia,” alisema Joel.

Hata hivyo, alikataa kutaja jina la mbunge huyo wala chama chake. “Siwezi kukuambia jina wala chama anachotoka," alisema Joel.

Hata hivyo, chanzo kimeidokeza NIPASHE kuwa mbunge huyo ni wa jimbo moja la Mkoa wa Rukwa.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mmoja wa baadhi ya wabunge ambao mbunge huyo hukaa nao jirani ndani ya ukumbi wa Bunge, alishauriwa kutokufanya hivyo, lakini alibisha.

“Tulimuona wakati akiandika barua ile na kuweka sahihi na tukamshauri tukamwambia Waziri Mkuu ana mamlaka ya juu sana huwezi kumfanyia mchezo halafu Selasini (Joseph Mbunge wa Rombo Chadema) si mtani wake, lakini yeye aliendelea na msimamo wake ndiyo yakampata haya,” alisema mbunge huyo. 

Jumatano iliyopita, muda mfupi kabla ya kuahirishwa kikao cha Bunge cha jioni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kuomba mwongozo wa Mwenyekiti wa Bunge kuhusu baadhi ya wabunge kuwaandikia wenzao barua wakitumia jina la WaziriMkuu Pinda.

”Mheshimiwa Mwenyekiti, umeibuka mtindo kwa baadhi ya waheshimiwa wabunge kuandika vimemo kwenda kwa wenzao wakiwahadaa kuwa wanaitwa na Waziri Mkuu kwa majadiliano muhimu. Vimemo hivyo hughushiwa jina na sahihi ya Waziri Mkuu. Hii si tabia nzuri hata kidogo.

Mfano wa sasa hivi Mheshimiwa Selesini aliandikiwa kimemo kama hicho na alipoinukana kumfuata Waziri Mkuu, alimkuta anafuatilia kwa makini hoja za Waziri wa Kilimo,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Ilibidi Mheshimiwa Selasini aendelee kusimama pale kwa adabu na kwa muda mrefu hadi Waziri Mkuu alipomwambia kuwa memo hiyo hakuandika yeye. Naomba mwongozo wako Mheshimiwa Mwenyekiti kwa suala hili.”

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits