Friday, July 1, 2011

Zito alianika Baraza la Mawaziri

Best Blogger Tips
Via Mwananchi

WAKATI Ofisi ya Bunge ikigoma kumsaidia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kupata nyaraka za Kikao cha Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kuthibitisha madai yake kuwa Baraza hilo limerubuniwa, mbunge huyo amewasilisha kurasa nne za ushahidi huo akitumia dokezo la kikao hicho cha siri.

Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel zilisema kuwa Zitto aliwasilisha ushahidi huo kwenye Ofisi ya Bunge jana mchana, huku taarifa zaidi zikionyesha kuwa aliwasilisha ushahidi huo ukiwa na hoja tatu kuthibitisha madai yake.

Kwa mujibu wa habari hizo, mbunge huyo aliwasilisha ushahidi wake uliosomeka “Tofauti kati ya mapendekezo ya Waraka wa Barazaa la Mawaziri na Pendekezo la Azimio la Bunge lililoletwa bungeni kuhusu kuongeza muda wa Shirika Hodhi la Mali za Mashnirika ya Umma, yaani Consolidated Holding Corporation (CHC)" .

"Amewasilisha ushahidi wake leo, uko hapa unafanyiwa kazi," alisema Joel alipoulizwa na gazeti hili.

Juzi, Spika Anne Makinda alimwongezea muda Zitto hadi Jumatatu Juni 4 mwaka huu, kuthibitisha madai yake hayo baada ya kueleza kuwa alishindwa kufanya hivyo juzi, Juni 29 kutokana na ofisi ya Spika kugoma kumsaidia kupata nyaraka za Kikao cha Baraza la Mawaziri kwa kuwa ni siri.

Akithibitisha hoja zake katika ushahidi huo ambao gazeti hili umefanikiwa kuuona, Zitto alisema, Azimio la Bunge lililowasilishwa bungeni na Serikali kabla ya marekebisho lilitaka CHC iongezewe muda wa mpito wa miaka mitatu na baadaye kazi zitakazokuwa zimebaki zipelekwe kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina ni tofauti na mapendekezo ya kitaalamu yaliyofikishwa mbele ya Baraza la Mawaziri.

Kwa mujibu wa maelezo ya Zitto, waraka wa wataalamu ulikuwa na mapendekezo ya aina mbili na kwamba hakuna hata pendekezo moja katika mapendekezo hayo lililozungumzia CHC kuongezewa muda wa miaka mitatu.

"Pendekezo la kwanza linalopatikana katika Aya ya 11.0 ya waraka huo, lilitaka CHC ifanywe kuwa taasisi ya kudumu. Pendekezo la pili linalopatikana katika Aya ya 12.0 ya waraka huo, liligusia mpango mbadala wa kuiongezea CHC muda wa miaka 5," ilisema sehemu ya ushahidi huo.

Katika ushahidi huo, Zitto alisema Aya ya sita ya Azimio la Bunge ilianza kujenga hoja ya kutaka CHC iongezewe muda wa mpito na baadaye majukumu yake yahamishiwe kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina. Alisema aya hiyo ilisomeka hivi:

"Na kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kuiongeza muda wa mpito wa shirika na Serikali inaandaa na kukamilisha utaratibu wa kuhamishia majukumu ya CHC kwenye Ofisi ya Hazina.

"Wakati Azimio lililoletwa bungeni lilijenga hoja hiyo ya kutaka majukumu ya CHC yaje kuhamishiwa kwenye ofisi ya Msajili wa Hazina, Waraka wa Baraza la Mawaziri katika pendekezo lake la pili, umetahadharisha kuwa mpango wa kuhamishia kazi za CHC kwenye ofisi ya Msajili wa Hazina, utakabiliwa na changamoto kubwa,"ilisema sehemu ya ushahidi huo.

Ushahidi wake huo kwenye hoja ya tatu ulisema kuwa, wakati Azimio hilo lililoletwa bungeni (kabla ya kurekebishwa) lilijikita katika kutaka CHC iongezewe miaka mitatu na baadaye majukumu yake yahamishiwe kwenye ofisi ya Msajili wa Hazina, hitimisho la waraka uliowasilishwa kwa Baraza la Mawaziri katika Aya ya 13 linasomeka:

"Waheshimiwa mawaziri, mnombwa kutafakari mapendekezo yaliyomo kwenye Aya ya 11 ya waraka huu na kumshauri Mheshimiwa Rais ayakubali na aagize utekelezaji wake

"Hivi ni dhahiri kuwa Baraza lamawaziri lilikiuka maoni na ushauri wa wadau na watalaamu wote waliotaka CHC ifanywe kuwa taasisi ya kudumu; na dhahiri kuwa Seriakli ilikiuka mapendekezo na sababu zake zote za msingi zilizowasilishwa katika kikao hicho ambazo zilitaka CHC ifanywe kuwa taasisi ya kudumu" inahitimisha taarifa hiyo.

Juni 23 mwaka huu wakati anachangia Azimio hilo, Zitto alisisitiza mara tatu kwamba Baraza la Mawaziri limerubuniwa kufikia hatua hiyo na akawataka wabunge kwa umoja wao kutokubali kupitisha azimio hilo kwa kuwa lipo kwa maslahi ya watu.

"Waheshimiwa wabunge, nawaombeni kwa umoja wetu tulikatae azimio hilo, hicho sicho tulichokubaliana kufanya. Tayari tumeiagiza CHC kufuatilia madeni yetu kwenye kampuni za umma halafu leo, tunataka kuliua shirika hili? alihoji Zitto kabla Spika Makinda hajamtaka athibitishe kauli hiyo.

Kadhalika, wakati Makinda akimwongezea Zitto muda wa kuthibitisha madai yake alisema “Waheshimiwa wabunge itakumbukwa kuwa tarehe 23 mwezi huu Mheshimiwa Zitto wakati akichangia Azimio la Serikali kutaka kuliongezea uhai Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC), alitoa tuhuma bungeni kwamba Baraza la Mawaziri, limerubuniwa kufikia maamuzi hayo."

Aliongeza: "Itakumbwa pia kuwa baada ya kauli hiyo, nilimtaka (Zitto) alete ushahidi ifikapo tarehe 29 Juni yaani leo. Sasa kwa kuwa siku yenyewe ya kuleta ushahidi ni leo, naona bora nitoe taarifa rasmi kwenu."

"Kwamba siku ileile ya tarehe 23, Mheshimiwa Zitto aliniandikia barua kuniomba nimsaidie kumpatia nyaraka za Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichopitisha uamuzi huo. Amefanya hivyo kwa kutumia Kanuni ya Haki, Sura na Madaraka ya Bunge zinazompa haki mbunge kuiomba ofisi ya umma kumpa nyaraka anazozihitaji.

Hata hivyo, Makinda alisema, ofisi yake haikuweza kumpatia Zitto nyaraka hizo kwa kuwa vikao vya Baraza la Mawaziri ni siri na nyaraka zake zote hazitolewi kwa umma.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits