Tuesday, July 5, 2011

Serikali yamsafisha rasmi Chenge

Best Blogger Tips
Via Tanzania daima

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiwa kimewaweka pabaya makada wake watatu kinaotaka kuwafukuza uongozi katika vikao vikuu vya chama katika dhana ya kukjivua gamba, serikali imemsafisha rasmi mmoja wao, Andrew Chenge, ikidai hauhusiki na kashfa anazotuhumiwa.

Chenge, ambaye amekuwa akihusishwa na ufisadi katika ununuzi wa rada nchini Uingereza, alisafishwa na serikali jana bungeni kwa kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, wakati akijibu hoja za wabunge kuhusu makadirio ya matumizi na mapato ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2011/2012.

Alisema Chenge hahusiki na kashfa ya ununuzi wa rada. Badala yake, serikali imewataja waliohusika katika tuhuma hizo kuwa ni dalali Sailesh Vithlani na vigogo wawili wa Kampuni ya BAE System ya Uingereza, inayotengeneza zana za kivita.

Alisema kwa mujibu wa Shirika la Uchunguzi wa Makosa Makubwa la Uingereza (SFO) na Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa nchini (TAKUKURU), Chenge hakuonekana sehemu yoyote kuhusika katika sakata hilo.

“Hakuna ushahidi kuhusu Chenge kuhusika na mchakato huo wa rada, hivyo hatuwezi kwenda mahakamani kwa hisia, ndiyo maana hadi leo tulikaa kimya,” alisema Chikawe.

Alisema suala la rada limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu na kwa namna mbalimbali, ikiwamo kupotoshwa, hivyo ikiwa kuna mtu ana ushahidi dhidi ya Chenge aupeleke kwa serikali ili wamshitaki haraka iwezekavyo.

“Kama hakuna ushahidi, ndiyo maana tunatangaza kama kanisani kuwa kama kuna mtu ana ushahidi na yanayosemwa alete, tutaushughulikia hata leo,” alisema Chikawe kwa kujiamini.

Hatua hiyo inachukuliwa wakati zikiwa zimebaki siku chache kwa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kukaa kujadili, pamoja na mambo mengine, kuwafukuza uongozi makada walioamuliwa kujiondoa wenyewe kwa tuhuma za ubadhirifu, ambao hadi sasa hawajajiondoa.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Bunge iliyotumwa kufuatilia fedha za rada imewasilisha ripoti yake kwa Spika jana mchana huku ikipendekeza waliohusika katika kashfa hiyo ya ununuzi wa rada wa Tanzania na Uingereza wachukuliwe hatua.

Mapendekezo hayo yalitolewa jana na mjumbe wa kamati iliyoundwa kufuatilia fedha hizo, Mussa Azzan Zungu, kwa niaba ya wenzake. Kwa niaba ya kamati, Naibu Spika Job Ndugai ndiye aliyemkabidhi Spika Anne Makinda ripoti hiyo.

Katika ziara ya Uingereza, mbali na Ndugai na Zungu, wajumbe wengine walikuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Angela Kairuki (CCM) na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP).

Kamati ilipendekeza pia kwamba ifikapo Septemba, kama BAE Systems itakuwa haijatekeleza matakwa ya kukabidhi pesa hizo serikalini, ishitakiwe.

Zungu alisema walipokuwa Uingereza walisisitiza kwamba pesa hizo si msaada bali ni haki ya Watanzania.

Alisema kwa sasa Bunge la Uingereza na serikali wanatambua mchezo mchafu uliofanywa na BAE kwa kutaka kulipa fedha zetu kwa kutumia asasi za kiraia. Alisema Serikali ya Uingreza imeona uonevu huo wa BAE Systems.

Awali Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Job Ndugai, alikiri kwamba walipokuwa Uingereza walikuwa wakihojiwa kama serikali imekwisha kuchukua hatua zozote dhidi ya watuhumiwa waliosababisha pesa hizo kuibwa. Alisema hii ndiyo ilikuwa changamoto kubwa waliyokumbana nayo.

Hata hivyo, alisema kuna ugumu katika kuwashughulikia wahusika, kwani BAE walikwisha kujiondoa katika kashfa hiyo na kesi ilikwishafungwa, wakajisafisha.

Kwa mujibu wa Ndugai, kamati za Kampuni ya BAE na SFO zinatarajiwa kubanwa na Kamati ya Bunge ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza kujibu tuhuma za sakata hilo la rada.

Ndugai alisema kikao hicho cha wazi cha pamoja kinatarajiwa kufanyika Julai 19 mwaka huu kwa kushirikiana na Wizara ya Sheria, Taasisi ya Rushwa ya Uingereza na wengine.

Kamati hiyo ilikwenda Uingereza Juni 17, 2011 na kurejea Juni 28, 2011 kushawishi BAE ilipe pauni milioni 29.9 na riba yake kupitia katika akaunti ya BAE zilikohifadhiwa.

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits