Friday, July 15, 2011

Kijana amuua mama yake kwa panga

Best Blogger Tips
Via Tanzania Daima

KIJANA mmoja mkazi wa kijiji cha Mgori, mkoani Singida, Miraji Joseph (22), anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumuua mama yake kwa kumchinja kwa kutumia panga na kisha kutenganisha kichwa na kiwiliwili.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari na kamanda wa polisi wa mkoa huo, Celina Kaluba, ilimtaja aliyeuawa kuwa ni Juliana Hango (57).

Taarifa hiyo iliongeza kuwa tukio hilo la kusikitisha lilitokea Julai 12, mwaka huu, majira ya saa 10.45 jioni katika kitongoji cha Mwamba.

Taarifa hiyo ilisema kuwa polisi walipata taarifa juu ya mauaji hayo kupitia kwa mtoto mwingine wa marehemu Adam Joseph anayefanya kazi ya ualimu katika Shule ya Msingi Mbusuruangiri, mkoani Shinyanga.

Joseph ambaye alikuwa katika mapumziko ya likizo mkoani Singida alishangaa kumkosa mama yake aliporejea katika shughuli zake.

Hata hivyo kamanda huyo alisema baada ya mwalimu huyo kumwuliza mtuhumiwa wa tukio hilo alikokwenda mama yao…alijibu kuwa hafahamu.

Taarifa hiyo ilisema kuwa Joseph aliamua kuzunguka nyuma ya nyumba na kugundua michirizi ya damu huku mwili wa mama yake ukiwa umechinjwa na kichwa chake kikiwa ndani ya boksi.

Katika eneo hilo walikuta panga likiwa na damu ambalo linasadikiwa kutumika katika tukio hilo.

Jeshi la polisi limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo na atafikishwa mahakamani wakati wo wote kujibu tuhuma hizo.

Taarifa ya awali ilidai kuwa inawezekana mtuhumiwa huyo alirudiwa na ugonjwa wake kutokana na siku za nyuma kuwahi kuugua ugonjwa wa akili (kichaa).


No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits