Friday, July 22, 2011

Hosea: Chenge ana kesi ya kujibu

Best Blogger Tips
Andrew Chenge
Via Mwananchi

SAKATA la kumiliki dola 1.2 milioni za Kimarekani (zaidi ya Sh1.2bilioni) katika kisiwa cha Jersey, Uingereza, linalomkabili mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, limeingia katika hatua mpya baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kutangaza kukamilisha uchunguzi na kukabidhi jalada kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kwa hatua zaidi za kisheria.

Chenge alikutwa na kiasi hicho cha fedha mwaka 2008, kufuatia uchunguzi wa kashfa ya ununuzi wa  rada uliofanywa na Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO).

Chenge ambaye wakati wa ununuzi huo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) anatuhumiwa kuwa kiungo muhimu katika ununuzi wa rada kati ya Serikali ya Tanzania na Kampuni ya BAE Systems.

Hata hivyo, kufuatia Chenge kukutwa na kiasi hicho kikubwa cha fedha zenye utata ambacho alikiita vijisenti, kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa watu wa kada tofauti nchini wakitaka ashitakiwe, na jana Mkurugenzi wa Takukuru Dk Edward Hoseah, alitangaza hadharani mjini Arusha kwamba mtuhumiwa huyo wa ufisadi atashtakiwa chini ya kifungu cha 27 Sheria ya Takukuru ya mwaka 2007.

Sehemu yakifungu hicho cha sheria, kinaainisha kuwa mtu akiwa na mali ambazo hazilingani na kipato chake alichokipata akiwa madarakani au baada ya kuondoka, ni kosa kisheria.


“Mtu ambaye atafanya kosa akiwa au akishikilia madaraka ya umma, kwa kuishi kwa kipato ambacho hakilingani na kipato cha sasa au kile alichopata…Au anayemiliki mali ambazo hazilingani na kipato chake kisheria, atakuwa akitenda kosa.” Kifungu hicho kinaeleza.

Dk Hoseah alifafanua zaidi kwamba,  kama DPP atalipitisha jalada hilo la Chenge, mbunge huyo atafikishwa mahakamani wakati wowote.

Kashfa ya kuwa na fedha hizo katika akaunti ya nje, ndiyo ilimwondoa Chenge katika wadhifa wa Uwaziri wa Miundombinu mwaka 2008, baada ya gazeti la Guardian la Uingereza kufichua kuwa Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali wa zamani, alikuwa akimiliki kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo, alipoulizwa na waandishi Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere baada ya kuachana na msafara wa Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa akitoka naye ziarani nchini China, Chenge alikiri kumiliki akiba hiyo ya fedha, lakini akiziita ni vijisenti, jambo ambalo liliwashangaza watu wengi nchini na kuibua hasira zaidi.

Lakini, Dk Hoseah akifafanua zaidi mchakato huo mzito wa kisheria, alisema ni Watanzania wachache mno wanaoweza kuwa na akiba ya fedha kiasi kama hicho nje ya nchi au mahali kokote, jambo ambalo aliongeza kuwa ndilo lililowasukuma kufanya uchunguzi kuhusu fedha hizo za Chenge.
Endelea kusoma habari hii.............................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits