Friday, July 15, 2011

Lowassa: Nimeshtushwa

Best Blogger Tips
Via Mwananchi

WAKATI uamuzi wa Rostam Aziz kung'atuka ubunge wa Igunga na ujumbe wa Halmashauri Kuu (Nec) ndani ya chama chake cha CCM ukiibua gumzo kubwa karibu kila kona nchini, mshirika wake mkubwa kisiasa, Edward Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli ameeleza kushtushwa na tukio hilo.Juzi, Rostam, mmoja wa watu muhimu ndani ya CCM aliyeshiriki vyema katika mtandao uliomwingiza madarakani Rais Jakaya Kikwete mwaka 2005, alitangaza uamuzi mzito wa kung'atuka siasa akipinga kile alichokiita siasa uchwara za baadhi ya viongozi wake.

Uamuzi huo mzito wa Rostam uliibua kwikwi na vilio kutoka kwa wapigakura jimboni kwake Igunga, wakiwamo wale waliomchagua kwa vipindi vitatu mfululizo tangu mwaka 1994 ulipofanyika uchaguzi mdogo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Charles Kabeho. Jana, Lowassa alisema: "Kwa kweli nimeshtushwa, nimesikitishwa...kilichonishtua zaidi ni vilio. Namna wananchi wa Igunga walivyokuwa wanalia na kusikitika."

Hata hivyo, Lowassa ambaye naye amekuwa akitajwa katika orodha ya watu watatu wanaopaswa kuachia nafasi zao za uongozi CCM katika kile kinachoitwa chama kujivua gamba, alipoulizwa kuhusu taarifa za yeye kufuata njia ya mshirika wake huyo alijibu: "Siku ikifika nitatoa uamuzi na nitajibu wakati ukifika."

Lowassa alikuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma, kuhusu alivyopokea uamuzi huo wa Rostam na kama yuko tayari kufuata mfano na njia hiyo ya kujiuzulu nyadhifa zote ndani ya CCM.
Lakini, juzi Rostam aliweka bayana kwamba uamuzi wake wa kujiuzulu hautokani na shinikizo lolote ikiwamo kile kinachoitwa mpango wa kujivua gamba, bali aliufanya uamuzi huo kuepuka kuathiri biashara zake kutokana na kuchafuliwa na siasa uchwara akieleza kuwa yeye ni mfanyabiashara wa kimataifa, lakini akaahidi kuendelea kuwa mwanachama mtiifu wa CCM.

Hata hivyo, Lowassa jana hakutaka kufafanua kuhusu kauli yake hiyo ya "Nitajibu wakati ukifika," ingawa alionyesha tabasamu wakati akiulizwa na kujibu swali hilo  la iwapo atafuata nyayo za Rostam au la.
Mshirika wao mwingine, Andrew Chenge, jana alivumishiwa kuandaa mkutano na waandishi wa habari  ili naye atangaze uamuzi wa kujiuzulu nafasi zake zote kama hatua ya kutekeleza azimio la Nec la kujivua gamba.

Lakini, alipotafutwa kwa simu na kuulizwa kuhusu taarifa za yeye kutaka kujiuzulu, Chenge alijibu kwa kifupi kuwa alikuwa Uingereza, kitu kilichothibitisha kuwa hakukuwa na mpango huo wa kujiuzulu huku akisisitiza: "Mimi niko nje ya nchi, nipo Uingereza."

Hivi karibuni, Chenge, Mbunge wa Bariadi Magharibi, maarufu kama Mzee wa Vijisenti, aliwahi kuliambia gazeti hili: "Sijui kama mimi ni gamba CCM," huku akisisitiza kwamba anaheshimu taratibu za chama na asingeweza kukurupuka na kuanza kuzungumza mambo ya chama nje ya utaratibu.
Chenge alisema chama kina utaratibu wake wa kufanya maamuzi, hivyo kuanza kutoka nje ya taratibu na kuzungumzia mambo ya ndani ya chama isingekuwa rahisi kwake kwani anaheshimu taratibu zilizopo.
Endelea kusoma habari hii.....................

No comments:


Copyright 2011 Mambo ya Leo Blog. All Rights Reserved.
 

yasmin lawsuits